Na Irene Clemence,Timesmajira
SERIKALI imeanzisha mfumo mpya wa mikondo miwili katika elimu ya sekondari ikiwa ni hatua ya mageuzi makubwa yenye lengo la kuongeza ubora wa elimu na kuwapa wanafunzi fursa ya kuchagua mkondo unaoendana na uwezo wao pamoja na malengo ya baadaye.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mapema leo Desemba 10,2025 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema kuanzia sasa wanafunzi watapewa nafasi ya kuchagua kati ya mkondo wa elimu ya jumla na mkondo wa elimu ya amali mara baada ya kumaliza elimu ya msingi, kwa ushauri wa wazazi na walimu.
Amesema mkondo wa elimu ya jumla utajikita zaidi katika masomo ya nadharia, kitaaluma na maandalizi ya vyuo vikuu, huku mkondo wa elimu ya amali ukielekezwa kwenye ujuzi wa vitendo, utendaji na maandalizi ya moja kwa moja katika soko la ajira.

“Lengo letu ni kuhakikisha kila mwanafunzi anapata nafasi ya kusoma kulingana na kipaji, uwezo na matarajio yake ya baadaye. Huu ni mwelekeo mpya wa elimu unaolenga kuongeza tija katika rasilimali watu,” amesema Prof. Mkenda.
Profesa Mkenda amesema kuwa mfumo huo pia utamwezesha mwanafunzi kubadili mkondo endapo atahitaji kufanya hivyo. “Mwanafunzi aliyepo katika mkondo wa amali anaweza kuendelea na kidato cha tano na sita katika mkondo wa elimu ya jumla iwapo atapenda na kufikia vigezo,” ameongeza.

Amesema wahitimu wa mkondo wa amali watapatiwa vyeti vinavyotambuliwa kitaifa na NACTVET pamoja na NECTA, hatua itakayowawezesha kuajiriwa, kujiajiri au kuanzisha biashara baada ya kumaliza masomo yao.

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina