Na Joyce Kasiki, Dodoma
SERIKALI imeanza utekelezaji wa miradi ya maji ya Gridi ya Taifa mkoani Katavi kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wengi zaidi, hususan katika maeneo yenye changamoto ya uhaba wa maji.
Hatua hiyo inalenga kuboresha maisha ya wananchi na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika mkoa huo.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Matthew Kundo, wakati akijibu swali la Mbunge wa Katavi, Thomas Maganga, bungeni jijini Dodoma aliyetaka kujua lini serikali itaanza kugekeleza miradi ya maji ya Gridi ya Taifa mkoani Katavi.
Alisema kwa mkoa wa Katavi Serikali imeanza kufanya upembuzi yakinifu wa mradi wa kutoa maji kutoka Ziwa Tanganyika, ambao ukikamilika utanufaisha idadi kubwa ya wananchi wa mkoa huo.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo alieleza kuwa Serikali imeanza pia ujenzi wa mradi wa miundombinu ya kutibu maji yanayotokana na Bwawa la Nsenkwa lililopo Wilaya ya Mlele.
Utekelezaji wa mradi huo umefikia wastani wa asilimia tano na unatarajiwa kunufaisha wananchi zaidi ya 68,426 wanaoishi katika vijiji 16 vya wilaya hiyo.
Akijibu swali la msingi la Mbunge Maganga kuhusu mpango wa Serikali wa kupeleka fedha kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa miundombinu ya kuchuja maji ya Bwawa la Nsenkwa, Mhandisi Kundo alisema Serikali itaendelea kupeleka fedha za utekelezaji wa mradi huo kadri zitakavyopatikana ili kuhakikisha unakamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi kwa wakati uliopangwa.
Katika swali la nyongeza, Maganga alitaka kujua hatua zinazochukuliwa na Serikali dhidi ya mkandarasi anayetekeleza mradi huo, kutokana na kasi ndogo ya utekelezaji wa kazi. Akijibu, Naibu Waziri alisema yupo tayari kufika eneo la mradi ili kujionea mwenendo wa ujenzi na kuchukua hatua stahiki endapo itabainika mradi hauendi kama ilivyokusudiwa.

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina