Na Mjuni Mwesigwa, TimesMajira,Online Dar
SERIKALI ameeleza jinsi maofisa wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) wakishirikiana na watu waliojitambulisha Polisi walivyofanya unyang’anyi wa sh. milioni 20 kutoka Kiwanda cha Smart kilichopo Kijitonyama jijini Dar es Salaam kwa madai kwamba kimekuwa kikizalisha bidhaa kwa kutumia malighafi zilizokwisha muda wake.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Makao Makuu ya TBS, Naibu Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, amewataka maofisa hao kuwa Afisa Viwango, Sulemain Banza, Ofisa Usafirishaji, Thomas Elisha na dereva, Issa Dodo.
Amesema watu hao walifika kiwandani hapo Februali 12, mwaka huu wakiwa na watu wengine waliojitambulisha ni Polisi wakitaka kufanya ukaguzi
Kwa mujibu wa naibu waziri, maofisa hao hawakuwa wametumwa na TBS na kwamba, Banza aliingilia majukumu ya watu wengine kwa kwenda kufanya ukaguzi kiwandani hapo, wakati kazi zake yeye ni afisa viwango na sio mkaguzi.
Aidha, amesema maofisa hao walitumia gari la Serikali kwenda kufanya unyang’anyi huo.
Kwa mujibu wa waibu Waziri, Kigahe mara baada ya kufika kiwandani hapo kwa nia ya kutaka kufanya ukaguzi, baadaye walitaka walipwe sh. milioni 100 ili wasiweze kumchukulia hatua mwenye kiwanda hicho, lakini hakuwa na kiasi hicho cha fedha.
Amesema baada ya hapo walitaka walipwe sh. milioni 50, ambazo nazo mwenye kiwanda hakuwa nazo ndipo walipotaka sh. milioni 20.
Amesema kwenye akaunti yake mwenye kiwanda hicho alikuwa na sh. milioni 10 na mke wake kwenye akaunti yake alikuwa na kiasi kama hicho.
Naibu Waziri Kigahe amesema mmiliki wa kiwanda hicho, mkewe na mhasibu waliwekwa chini ya ulinzi wa watu waliojitambulisha ni Polisi na kuondoka nao hadi benki, huku wakiwa wamenyang’anywa simu na kuwasimamia watoe fedha hizo benki.
Amesema baada ya kutoa fedha hizo kiasi cha sh. milioni 20, waliwaachia watu hao na kuwarudishia simu zao ndipo walipopiga simu wizarani na kutoa taarifa za tukio hilo.
Amesema kitendo kilichofanywa na watumishi hao wa TBS ni unyang’anyi na uporaji wa hali ya juu kwa sababu Serikali haikuwatuma, bali walijituma wenyewe kwenda kuwasumbua wawekezaji waliowekeza nchini kwa ajili ya kuliingiza mapato taifa na kutoa ajira kwa Watanzania.
Kufuatia kitendo hicho, Kigahe ameagiza kusimamishwa kazi maofisa hao na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) kwa kushirikiana na Polisi kufanya uchunguzi dhidi yao ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.
More Stories
DC Korogwe awataka viongozi wa vijiji kuwatumikia wananchi kwa uadilifu
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam