Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
SERIKALI imeeleza dhamira yake ya kuendelea kutafuta na kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara muhimu mkoani Pwani, zikiwemo barabara za Mzenga–Kisarawe na Chalinze–Utete, kutokana na mchango wake katika kukuza uchumi wa wananchi na kuimarisha mawasiliano ya maeneo ya jirani.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni na Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya, wakati akijibu swali la Mbunge wa Kisarawe Dkt.Selemani Jafo.
Katika swali lake Jafo alihoji mpango wa serikali kutenga fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa barabara ya Mzenga–Kisarawe yenye urefu wa kilometa 70 kwa kiwango cha lami.
Mhandisi Kasekenya alisema serikali inatambua umuhimu wa barabara hiyo na inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya utekelezaji wake.
Alisema ujenzi wa barabara hiyo utachochea shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa Wilaya ya Kisarawe, Mkoa wa Pwani na maeneo ya jirani.
“Tutaendelea kuongeza fedha kadri zitakavyopatikana ili kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami, kutokana na umuhimu wake kwa maendeleo ya wananchi,” alisema Kasekenya.
Naye , Mbunge wa Kibaha Vijijini (CCM), Hamoud Jumaa, alitaka kujua mpango wa serikali wa kujenga barabara ya Chalinze–Gwata–Magindu–Mpalu–Utete–Rufiji–Tumbi–Boko–Sofa pamoja na Korogwe–Sofa.
Akijibu, Mhandisi Kasekenya alisema serikali ipo katika hatua za manunuzi ya kumpata mshauri atakayefanya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi wa barabara mpya ya Chalinze hadi Utete yenye urefu wa kilometa 354.9, itakayopita katika eneo la Bwawa la Julius Nyerere la Kufua Umeme (NHPP).
Aliongeza kuwa usanifu huo unajumuisha kipande cha barabara ya Chalinze hadi Magindu chenye urefu wa kilometa 22.61, na baada ya kukamilika kwa usanifu na kubainika kwa gharama za ujenzi, serikali itaanza mchakato wa kutafuta fedha ili kuanza utekelezaji wa mradi huo.

More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama