Na Judith Ferdinand, Mwanza
HALMASHAURI zote nchini pamoja na taasisi za Serikali zimetakiwa kuhakikisha maeneo yao yanakuwa na hati miliki kwa mujibu wa sheria huku ikipigwa marufuku vitendo vya watu kuchukua maeneo ya wananchi bila kuwalipa fidia zao.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Dkt.Angeline Mabula katika Baraza Maalum la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani hapa la kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa 2018/2019 lililofanyika mjini hapa.
Baraza hilo limehudhuriwa na Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza,Emmanuel Tutuba aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella.
Dkt.Mabula amesema,wizara imeelekeza halmashauri zote nchini na taasisi zote za Serikali kuhakikisha kuwa wanamilikishwa maeneo yao kisheria ili kuondoa migogoro na siyo kubaki tu kusema kwamba hii ni mali yangu na mwisho wa siku inaonekana migogoro inaongezeka.
“Mimi niseme tubadilike katika masuala ya ardhi itambulike kuwa eneo hili ni mali ya taasisi za umma kwa kuwa na hati miliki kwa mujibu wa sheria ili kuondoa migogoro,pia katika masuala ya ardhi na sisi tunasema ni marufuku mtu kuchukua eneo la mtu mwingine bila kuwalipa fidia,nishukuru wizara husika imejaribu kuzipigia debe na kuweza kupata fidia zao wananchi,maeneo yanapojengwa shule za sekondari za kata, tunapochukua maeneo niseme lazima ushirikishwaji uwepo,”amesema Dkt.Mabula.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kawekamo, Japhes Rwehumbiza amesema, hawana sababu ya kuchukua kipande cha ardhi ya mwananchi na kukipima bila kumlipa fidia, kwani hayo yamekuwa yakiwaletea matatizo kwenye baraza lao ambalo linaenda kuisha muda wake.
“Na sisi tunatoa rai pamoja na kuwa tunaenda kumaliza kipindi chetu,CAG na wale waliobaki waendelee kutekeleza maelekezo ya Naibu Waziri wa Ardhi na Baraza la Madiwani kwamba tusichukue maeneo ya watu pasipo kuwalipa jasho lao,ile ardhi imetunzwa,ile ardhi imeendelezwa unakuta kuna miti kila aina ya mazao na bila kuwalipa fidia tunakuwa tunawarudisha nyuma, hivyo kuona Serikali yao mbaya,”amesema.
Naye Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Renatus Mlunga amesema ukiulizwa Ilemela ni nini jibu elimu,hivyo ili kuweza kuendana na matumizi mazuri ya ardhi na kuepuka migogoro halmashauri hiyo inabidi kujenga shule zenye majengo ya kwenda juu, ghorofa na kuacha yale ya kusambaa.
More Stories
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari
Gridi za Tanzania, Kenya kuimarisha upatikanaji wa umeme
Mama Zainab:Watoto yatima ni jukumu la jamii yote