Na Mwandishi wetu,Timesmajiraonline,
Balozi wa Tanzania Nchini Malawi, Humphrey Polepole ameshiriki katika zoezi la kukabidhi misaada ya Kibinadamu kutoka Tanzania kwa Serikali ya Malawi ili kusaidia waathirika wa Kimbunga Freddy.
Balozi Polepole amekabidhi misaada hiyo ya kibinadamu inayojumuisha Mablanket, Mahema, Unga wa Mahindi kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi, Nancy Tembo katika Mji wa Blantrey Nchini Malawi mapema leo 25/03/2023.
Polepole ameeleza kuwa wa watanzania, na watu wa Malawi ni jamii moja na nia ya kutoa misaada hiyo ni kuendeleza umoja uliojengwa na waasisi wa Nchi zetu.
“Msaada huu wa kibinadamu utasaidia, katika jitihada za kurejesha matumaini na ustawi kwa ndugu zetu wananchi wa Malawi”,amesema Balozi Polepole.
Aidha amesema kuwa ana imani na wapiganaji wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania walikwenda nchini Malawi watashirikiana na wenzao Wanajeshi wa Malawi, kuhakikisha kwamba misaada iliyotolewa inawafikia waathirika wa Kimbunga hicho.
“Tanzania imetoa madawa ya binadamu, ambayo yataweza kusaidia kwenye maeneo ambayo vituo vya afya vimeathirika. Hizi zote ni jitihada za kusaidia Nchi ya Malawi katika kurejesha huduma za afya,
“Tunamshukuru sana Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa Msaada aliotoa kwa Nchi ya Malawi, kwa uwezeshaji wa fedha na wapiganaji wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (Wahandisi wa Medani) ambao watasaidia katika kurejesha hali ya miundo mbinu Nchini Malawi,”amesema Balozi.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya nje wa Nchi ya Malawi Nancy Tembo amesema ameshukuru Nchi ya Tanzania kwa Msaada wa kibinadamu iliowapatia, ambao umefika katika wakati muafaka.
“Msaada huu ni muhimu kwetu kwa sababu tunao Wananchi wengi ambao makazi yao yameharibika na tunahitaji msaada wa kila mtu ili kuhakikisha waathirika wa Kimbunga Freddy wanapatiwa huduma za msingi kwa wakati,”amesema Waziri Nancy
Pia amesema kuwa Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania wamekuja kutusaidia na wataungana na askari wetu wa Nchini Malawi katika kurudisha miundombinu iliyoharibika katika hali ya kawaida.
“Nachukua fursa hii kumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutusaidia katika wakati ambao tunahitaji msaada sana, janga hili ambalo limeathiri Nchi ya Malawi, limegharimu maisha ya watu, na limeharibu miundombinu,”amesema Waziri Nancy.
Naye Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulika na Operesheni pamoja na Uratibu wa shughuli za Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge Uratibu Luteni Kanali Selestine Masalamado ametoa pole kwa wananchi wa Malawi kwa Maafa ya Kimbunga Freddy.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alielekeza Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Maafa kuratibu swala la misaada ya kibinadamu kwa ajili ya waathirika wa Kimbunga Freddy Nchini Malawi, ambapo kwa awamu ya kwanza helikopta mbili kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania zilisafiri kuja Malawi kufanya kazi za wokozi, lakini msaada wa pili ilikuwa ni msaada wa fedha kwa serikali ya Malawi na tatu ni kutoa msaada wa kibinadamu kwa Wahanga wa Kimbunga Freddy,”ameeleza luteni Kanali Masalamado.
More Stories
Tanzania,Uturuki kushirikiana kuinua sekta ya utalii nchini
Wanaoficha watoto wenye ulemavu kusakwa
Mawakili Tabora walaani kuziwa kutekeleza majukumu