Na Joyce Kasiki,Timesmajira ,Dodoma
SERIKALI ya Nchini Canada imetangaza kutoa kiasi cha Dola za Canada milioni 50 sawa na Shilingi Bilioni 93.14 za Kitanzania kwa ajili ya utekelezaji wa miradi miwili ya kila binti asome na uwezeshwaji kupitia programu za ujuzi unayolenga kuwakwamua vijana wa Kitanzania kiuchumi.
Hayo yamejiri wakati Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa nchini Canada Harjit Sajjan alipofanya ziara katika Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia iliyolenga kueleza kusuduio hilo huku Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda akipongeza hatua hiyo .
Waziri Mkenda amesema uamuzi huo umekuja wakati muafaka ambao Tanzania ipo katika mageuzi makubwa ya elimu huku mwelekeo ukiwa katika mafunzo ya amali.
“Hivi sasa Tanzania inafanya mageuzi makubwa ya elimu ambapo kwa sasa elimu yetu ya lazima ni miaka sasa,lakini katika mageuzi yake elimu yetu ya lazima itakuwa ni miaka kumi “amesema Profesa Mkenda na kuongeza kuwa
“Kwa hiyo hatua ya kwanza ni kuwa na elimu ya lazima ya miaka kumi badala ya miaka saba ya sasa,na tutakuwa na mikondo miwili ambayo ni elimu ya jumla na elimu ya mafunzo ya amali ambayo hii italenga ujuzi zaidi na masomo machache ya darasani,lengo ni kuhakikisha mtoto anapomaliza miaka kumi ya elimu ya lazima anakuwa na uwezo wa kuajiriwa ama kujiari mwenyewe na hivyo kujikwamua kiuchumi bila kutegemea ajira ya serikali.”amesema Profesa Mkenda
Akizungumza na Menejimenti ya Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia Waziri Harjit Sajjan amesema kati ya fedha hizo Dola za Canada milioni 25 (zaidi ya shilingi bilioni 46)ni kwa ajili ya kuboresha upatikanaji wa fursa za elimu na ujuzi kwa mabinti wa Tanzania, kukuza uwezeshaji wake na kupata fursa za ajira za staha.
Aidha amesema Dola za Canada nyingine milioni 25 ni kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa Kila Binti Asome miradi ambayo yote kwa pamoja imelenga kuwakwamua vijana katika suala zima la ajira.
Sajjan amesema,uwekezaji katika elimu ya wasichana hubadilisha jamii ,huimarisha uchumi na kupunguza ukosefu wa usawa lakini pia inachangia jamii kuwa imara zaidi na kutoa fursa kwa watu wote ikiwa ni pamoja na wavulana na wanaume.
“Sera yetu ya Usaidizi wa Kimataifa inaweka msisitizo katika fursa sawa kwa wanawake na wasichana hivyo kuna haja ya kuwa na mbinu iliyoratibiwa ili kuondoa hasara katika kujifunza”amesema Sajjan
Aidha amesema,Canada inajivunia kushirikiana na mashirika ,walimu na shule katika kufanikisha kwa uhalisia wa mfumo na huduma za elimu zinazozingatia jinsia ndiyo maana leo ninatangaza Dola za Canada milioni 25 kwa mradi wa Kila Binti Asome ambao utatekelezwa ka upande wa Tanzania Bara na Zanzibar chini ya Shirika la Kuhudumia Watoto (UNICEF).
“Mradi huu utawezesha elimu kwa mabinti katika ngazi ya msingi na sekondari ,haswa katika masomo ya Hisabati na Sayansi,itachangia kuongeza viwango vya vya uhitimu kwa wasichana katika shule za sekondari.”amesisitiza Waziri Sajjan
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato