Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
WADAU wa sekta ya ngozi pamoja na Serikali wameadhimia mambo 16 kwa ajili ya kuboresha na kuongeza thamani ya zao la ngozi ili kuleta tija katika sekta ya viwanda pamoja na kuchangia uchumi wa kati wa Taifa.
Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na kuwa na madaraja ya ngozi kuanzia la kwanza mpaka la nne, Wizara ya Mifugo kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa ajili ya majosho, kutoa elimu juu ya ubora wa ngozi ili wadau waweze kujua thamani ya zao la ngozi, Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia Tantrade na kutengeneza masoko ndani na nje ya nchi, kutumia teknolojia bora na machinjio ya kisasa.
Akizungumza baada ya kufunguliwa kwa kikao cha wadau wa sekta ya ngozi kilichofanyika Mkoani Mwanza, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Profesa Elisante Gabriel amesema, ubora wa ngozi unaanzia kwenye uzalishaji hivyo wao kama Wizara kwa kupitia taasisi yao ya utafiti (TARIRI) wanafanya kazi kubwa ya kuona kuwa kwa namna gani wanaboresha na kupata mbuzi wakubwa ili waliowekeza katika viwanda vya ngozi wasikose malighafi.
Kwa upande wa malighafi, Tanzania ina mifugo mingi lakini changamoto ni namna gani bora ya malighafi yenyewe hivyo jukumu la Wizara hiyo katika sekta ya mifugo ni kuhakikisha kuwepo na ngozi kubwa za kutosha na zenye ubora, kutumia teknolojia ya kisasa ili kutoa bidhaa zenye ubora,kusimamia sekta hiyo na kushiriki kulinda ubora wa ngozi.
“Kwanza ubora wa ngozi unaanzia kwenye jinsi mimba inavyo tungwa na ndio maana ndio sasa tunapandisha ng’ombe kwa njia ya mbegu,tunahakikisha mifugo hii inatibiwa vizuri kwa maana ya uogeshaji lakini pia kupata chanjo stahili kuhakikisha ngozi inakuwa bora,”.
“Wizara tumeisha endesha mafunzo na kusajili wachunaji zaidi ya 775 ambao tumewapa vifaa kama visu ili kuona ule uchunaji unakuwa bora sababu mnyama anaweza kuwa bora tatizo likaja kwenye uchunaji, anachunwa vipi anapo wekewa matobo na kukatwa katwa nalo linakuwa ni tatizo, kuna namna ya kuchuna mnyama na tupate ngozi bora,” amesema Profesa Gabriel.
Amesema, lazima pia kuwe na masoko ya bidhaa za ngozi kwani yanapopatikana masoko hayo hata ufugaji utaenda vizuri lakini pia hata wawekezaji watawekeza vizuri na hadi sasa wanahakikisha uogeshaji wa wanyama unaendelea.
Amesema, ndani ya wiki mbili zijazo watazindua kampeni ya tatu ambayo watafikia Mikoa 25 ambayo ina masuala ya mifugo na majosho ndani ya Halmashauri 161 na tayari wameishapata mkandarasi wa kuwauzia dawa kwa ajili ya kuogeshea mifugo hivyo wanasema masuala ya afya ya mifugo imepewa kipaumbele.
“Sasa hivi ni kuhakikisha tunapata ngozi nyingi na yenye ubora hivyo watanzania wajenge utamaduni wa kutimia bidhaa za ngozi zilizotengenezwa Tanzania na wajivunie, tukitumia bidhaa zetu soko litakuwepo na uzalishaji utaongezeka biashara ina kanuni zake bei inapangwa kutokana na gharama iliotumika hivyo wadau waliowekeza katika sekta hii wahakikishe bei ya bidhaa iwe tofauti tofauti kwani kuna wateja saba katika soko la kawaida, tusitake bei rahisi bali bei shindani,” amesema Profesa Gabriel.
Pia amesema kuwa, wameanza kuboresha machinjio,huku nchini kuna viwanda 32 vya viatu ambavyo vinauwezo wa kuzalisha jozi milioni 60 kwa mwaka na waagiza viatu kutoka nje jozi milioni 52 kwa mwaka.
Kwa upande wake Waziri wa nchi ofisi ya waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira, Vijana na Watu wenye ulemavu, Jenista Mhagama amesema sekta ya viwanda ina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa kati hivyo wenye viwanda vya ngozi nchini kutumia malighafi na kemikali zenye kiwango na ubora ili kukuza soko la bidhaa za ngozi ndani na nje ya nchi pamoja na kuwa na mpango endelevu wa kuhakikisha malighafi za ngozi zinapatikana kwa ubora unaotakiwa.
Mkurungezi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) Hosea Kashimba, amesema wapo na wadau wa sekta ya ngozi ili kuona kiwanda chao ambacho PSSSF wanamiliki asilimia 86 huku Jeshi la Magereza ambalo ni wabia lina asilimia 14 cha Kilimanjaro International Leather Industries Campany,kiweze kupata malighafi kutoka hapa nchini.
Kashimba amesema, ni kiwanda kikubwa cha aina yake na mfano nchini na Afrika Mashariki na Kati kinatarajia kutoa ajira kwa watanzania zaidi ya 7,000 kuzalisha viatu wastani wa juu jozi milioni 2.4 kwa mwaka na kiwango cha chini jozi milioni 1.2 kwa mwaka, pia kitatengeneza mikanda, pochi na makoti ya ngozi, kuchakata ngozi qubi futi milioni 15 kwa mwaka,itasaidia kuchakata ngozi kutoka kwa wafugaji wa pande zote nchini na tutaondokana na tatizo la kutupa ngozi kwa sasa na kitakuwa na faida katika uchumi wa Taifa.
“Hii yote ni katika kutekeleza maelekezo ya Serikali yetu,katika kuleta Serikali kwenye uchumi wa viwanda na wenye tija kubwa kwa kutumia malighafi za watanzania, na mtazamo ni kuwa na viwanda vingi viatu na kiwanda cha ngozi ni moja ya viwanda ambavyo wamewekeza na kwa historia kiwanda hiki cha ngozi ndicho kilichotumika kutengeneza viatu wakati wa vita ya Idd Amin mwaka 1979 hivyo wameenzi juhudi za Mwalimu Nyerere,” amesema Kasimba.
Hata hivyo Mwenyekiti wa Umoja wa Wanunuzi wa ngozi na waboreshaji(UWANGOTA) Abeid Matiko amesema, ubora wa ngozi bado ni changamoto hivyo wale wanaosimamia kwenye minada wahakikishe chapa kwenye mifugo inapigwa sehemu husika kama yalivyo maelekezo ya Wizara ya Mifugo, magonjwa ya mifugo yatibiwe kwa wakati na kuhakikisha inaoshwa kila wakati pamoja na kuanza maandalizi mapema kuhakikisha ngozi inaboreshwa kabla ya kiwanda hicho kuanza kazi.
Aidha Mtafiti kutoka Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) Cecilia China amesema, lengo ni kuongeza mnyororo wa thamani katika kusaidia ngozi hivyo changamoto iliopo ni ukosefu wa maabara za kufanyia utafiti wa ngozi mpaka watume sampuli nje ya nchi hivyo Serikali iwezeshe upatikanaji wa maabara hizo.
More Stories
Muhoji Sekondari kumaliza changamoto ya umbali kwa wanafunzi Musoma vijijini
Tanzania mwenyeji mkutano wa nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika
TANESCO yarudisha shukrani kwa jamii