November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali na Mashirika ya Umoja wa Mataifa wakutana Dodoma

Na Farida Ramadhan WFM- Dodoma

Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa (UN) wapo katika hatua za mwisho za maandalizi ya Mpango mpya wa Ushirikiano wa miaka mitano (United Nations Sustainable Development Cooperation Framework – UNSDCF) utakaoanza  mwaka 2022  hadi  mwaka 2027.

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Emmanuel Tutuba wakati wa ufunguzi wa Kikao cha Kamati ya Usimamizi wa Mpango wa Pili wa Ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Mashirika ya Umoja wa Mataifa (UNDAP II) uliofanyika jijini Dodoma.

“Katika Mpango huo mpya kuna maeneo mbalimbali yatakayo shughulikiwa ikiwemo Afya, Maendeleo ya Jamii, Uhimilivu wa changamoto mbalimbali za Maendeleo, ukuaji wa uchumi, demokrasia na utawala bora pamoja na Haki za Binadamu pamoja na masuala ya jinsia”, alisema Tutuba

Alisema katika maeneo hayo Serikali na UN watajadiliana ili kuona namna bora ya kuweka ustawi wa Watanzania kwa kuhakikisha Mpango wa tatu Maendeleo wa Miaka Mitano unafanikiwa ili kuleta maendeleo nchini.

Tutuba aliushukuru Umoja wa Mataifa kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza Sera za Uchumi ili kuharakisha ukuaji wa uchumi, kupunguza umaskini na kuboresha masuala ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi.

“Mchango wa UN na Wadau wengine wa Maendeleo tunautambua ni mchango mkubwa, hata tulivyoingia kwenye nchi yenye hadhi ya uchumi wa kati pia palikuwepo na mchango mkubwa kutoka kwao. Michango yao kupitia sekta mbalimbali imewezesha uchumi wetu kukua kwa kiwango cha asilimia 6 – 7 kwa miongo miwili iliyopita”, alibainisha Tutuba

Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini, Bw. Zlatan Milisic alisema Mpango huu mpya utabadilisha mfumo wa UN kushirikiana na nchi kwa kuhamasisha ushirikiano kwa kutekeleza shughuli za maendeleo na kuwaleta pamoja wadau wengi ili kuharakisha Maendeleo na kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

Aliahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutekeleza shughuli mbalimbali zinazoendelea katika kuhakikisha mpango huo unakamilika.

Kikao cha Kamati ya Pamoja ya Usimamizi wa Mpango wa Pili wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Umoja wa Mataifa (UNDAP II) wa mwaka 2016 – 2022 ni kikao cha maamuzi ya juu ambacho kinaongozwa na kwa pamoja kati ya Katibu Mkuu wa Hazina na Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa.