December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kuzindua mfumo wa malipo kielekitroniki wa CHF Iliyoboreshwa

Na Zena Mohamed, Timesmajiraonline, Morogoro.

SERIKALI ya Tanzania kuzindua mfumo wa malipo ya kielektroniki wa CHF-iliyoboreshwa utakaotumika nchi nzima ili kurahisisha namna ya kulipia michango ya uanachama na kupunguza gharama zinazoambatana na ukusanyaji wa fedha za mfuko huo.

Akiongea katika mafunzo rejea ya siku tatu ya matumizi ya mfumo huo wa kielekitroniki kwa timu za uratibu wa mfuko wa CHF Iliyoboreshwa yaliyofanyika Mkoani Morogoro hivi karibuni, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe katika Ofisi ya Rais – Tamisemi, Rasheed Maftah, aliwaelekeza kuhakikisha  wanafanya mafunzo rejea ya matumizi ya Mfumo huo kwa Timu za Uratibu wa CHF Iliyoboreshwa za Halmashauri, Wasimamizi ngazi za Kata na Maafisa Waandikishaji/Mawakala ngazi za Vijiji/Mitaa kabla ya  Januari 10 2022.

Mafta amesema katika mwendelezo wa jitihada za kuimarisha bima ya afya ya CHF iliyoboreshwa, kurahisisha namna ya kulipia kutaleta imani kwa wanachama kuhusu michango yao ndio maana  Serikali imezindua mfumo wa kielekitroniki wa kukusanya michango ya wanachama wa CHF Iliyoboreshwa ambao kwasasa una wanachama Zaidi ya Milioni 1.

“Ofisi ya Rais – Tamisemi, inaishukuru Wizara ya Fedha na Mipango (MoFP) na Wadau wa Maendeleo HPSS- Tuimarishe Afya kwa kufanikisha kukamilika kwa mfumo huu utakaowezesha ukusanyaji wa michango ya wanachama wa CHF Iliyoboreshwa kielektroniki uliounganishwa na Mfumo wa “Government e-Payment Gateway System (GePG)”, amesema Maftah.

Ameeleza kuwa Serikali imekuwa ikisisitiza matumizi ya mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji na usimamizi wa fedha za umma hivyo ili kuhakikisha makusanyo ya CHF-Iliyoboreshwa yanasimamiwa ipasavyo kwa kufuata kanuni za usimamizi wa fedha za serikali, haja ya kuandaa na kutekeleza mfumo wa malipo wa kielektroniki wa CHF-Iliyoboreshwa ni muhimu.

Amesema ili kufanikisha azma hiyo, Ofisi ya Rais- TAMISEMI kwa kushirikiana na Mradi wa HPSS- Tuimarishe Afya na Wizara ya Fedha na Mipango iliamua kuanzisha na kuwezesha uundaji wa mfumo wa malipo ya kielektroniki kwa CHF iliyoboreshwa utakaowezesha ukusanyaji wa malipo ya CHF kwa njia ya mitandao mbalimbali ya simu na benki.

Amesema Mradi HPSS-Tuimarishe Afya, unaofadhiliwa na Serikali ya Uswisi kupitia Shirika la Maendeleo na Ushirikiano la Uswisi (SDC) na kutekelezwa na Taasisi ya Uswisi Tropical and Public Health Institute kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI uliwezesha mafunzo hayo ya siku tatu kwa viongozi wa Serikali kuhusu mfumo wa malipo ya kielektroniki (e-payment) wa CHF iliyoboreshwa.

Ametaja Lengo kuu la mafunzo hayo kuwa ni kutambulisha mfumo wa malipo ya kielektroniki wa CHF-Iliyoboreshwa kwa maafisa husika wa serikali na kuongeza uelewa wao kabla ya kuanza kutekelezwa nchi nzima.

“Haya yanajiri baada ya kukamilika kwa mchakato muhimu wa kusanifu mfumo huo, kuuingiza katika Mfumo wa Serikali wa Kulipa Kielektroniki (GePG) na kufanyika kwa zoezi la majaribio lililofanyika mkoani Shinyanga kwa mafanikio makubwa,”amesema.

Amesema Mfumo wa GePG unasimamiwa na Wizara ya Fedha na Mipango kiufundi na kiundeshaji, na upo kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Umma (PFA) ya mwaka 2001 kupitia marekebisho ya mwaka 2017 (Sura 348), na Waraka wa HAZINA Namba 3 wa mwaka 2017. Sheria ya Fedha za Umma inawataka Maafisa Masuuli wote kukusanya fedha za Umma kwa kupitia Mfumo wa GePG

Aidha amesema Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ulianzishwa na Serikali kwa sheria ya mwaka 2001, ambapo kila Halmashauri ilitakiwa kuanzisha Mfuko huo huku tathmini ya uendeshaji wa mfuko huu ilionesha kwamba utekelezaji wake ulikuwa unakabiliwa na changamoto mbalimbali za kimuundo na kiuendeshaji.

Ameeleza kuwa Kufuatia changamoto hizo Serikali kwakushirikiana na wadau wa maendeleo imedhamiria kufanya maboresho katika maeneo matatu ili kuimarisha uendeshaji wa Mfuko wa CHF. Maeneo hayo ni; Usimamizi na Uendeshaji (Governance),Usajili wa wanachama wa Mfuko (Enrolment), Kitita cha mafao na ngazi ya upatikanaji wa huduma za Afya (Benefit Package).

“Moja ya vipaumbele vya serikali ni kuhakikisha kwamba wananchi wote wanapata matibabu kupitia mifumo ya bima za afya hasa wananchi walioko katika sekta isiyokuwa rasmi ili kufikia lengo la afya bora kwa wote, pia kusimamia ukusanyaji na  upatikanaji wa fedha, kutoa huduma zilizo bora zenye gharama nafuu na Kuboresha huduma za afya katika jamii,

“Ili kufanikisha azma hiyo Ofisi ya Raisi – TAMISEMI na Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Mradi wa HPSS – Tuimarishe Afya wanaendelea kufanya maboresho mbalimbali kwa kuleta mfumo mpya wa CHF iliyoboreshwa, ambao unatekelezwa kwa kupitia Waraka Namba 1 wa Maboresho ya Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF/TIKA).

Kwaupande wake,Elizeus Rwezaula kutoka Mradi wa HPSS- Tuimarishe Afya amesema mradi huo ambao umekuwa ukisaidia mipango bunifu ya afya ya serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Ofisi ya Rais-TAMISEMI tangu mwaka 2011 umejizatiti kuendelea kutoa msaada wa kiufundi katika mipango mbalimbali ya afya ikiwa ni pamoja na CHF-Iliyoboreshwa.

“Tunawashukuru washiriki wote wa mafunzo haya kwa michango yenu ambayo itasaidia kuboresha mfumo wa malipo ya kielektroniki wa CHF Iliyoboreshwa na tunaahidi kuendelea kutoa msaada wa kiufundi wakati wa utekelezaji wa mfumo huo”, amesema Rwezaula.

Mafunzo hayo yalishirikisha Waratibu wa CHF-Iliyoboreshwa katika ngazi ya mkoa, Maafisa TEHAMA na timu za CHF za Halmashauri kutoka nchi nzima.