November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kuwachukulia hatua watoroshaji wa mbolea ya ruzuku

Na Moses Ng’wat,Timesmajiraonline,Ileje

WAZIRI Mkuu,Kassimu Majaliwa, amesema serikali itaendelea kuchukua hatua kali zaidi kwa watu wanaotorosha mbolea ya ruzuku kupeleka nchi jirani kwasababu wanaofanya hivyo hawana tofauti na wauaji.

Akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Ileje katika siku ya kwanza ya ziara yake ya siku tatu mkoani Songwe,amesema mbolea imepanda bei duniani kote ndio maana serikali iliamua kutenga Sh.bilioni 50 kwa ajili ya kuweka ruzuku kwenye mbolea ili wananchi waweze kuinunua kwa bei nafuu.

“Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan alilipia kwa kuongeza ruzuku kwenye mbolea kwani leo mbolea duniani imepanda hivyo aliona watanzania hawatamudu kununua mbolea na hivyo alichofanya alitenga Sh.bilioni 50 ili kukuongezea wewe kwa mfuko utakaonunua kwa kuongezea Sh. 50,000 ili mkulima anunue kwa Sh.70,000 tu badala ya Sh.120,000,”alisema.

“Sasa wewe unayesafirisha mbolea kutoka Ileje kupeleka nchi jirani na kuuza wewe huna tofauti na muuaji kwasababu kwanza unachukua mbolea ya watanzania unapeleka mifuko 100 Malawi wakati hela ya watanzania imeingizwa kwenye mbolea hiyo,”amesema.

Majaliwa amesema serikali inaongeza ruzuku kwenye mbolea ili kuwawezesha wakulima wazalishe zaidi hivyo inapotokea kuna mtu anatorosha mbolea nje unataka watanzania wasizalishe wapate shida ya njaa wafe ndio maaana mtu anayefanya hivyo hana tofauti na muuaji.

“Wale mliowakamata kutoka Ileje mwaka juzi na mwaka jana mnaendelea kuwachukulia hatua kali na tutakaowashika mwaka huu hatua zitakuwa kali zaidi na muuaji nchi hii hakubariki,”amesema.

Majaliwa amesema Mkoa wa Songwe unaongoza kwa uzalishaji na hivyo mkakati wa serikali ni kutaka kuhakikisha uzalishaji unaongezeke zaidi.