Na David John,Timesmajira,Online
SEERIKALI ya Tanzania imetuma ujumbe wake katika Kongamano la Usawa wa Kijinsia, ambalo linatajia kufanyika kuanzia leo hadi Julai 2 mwaka huu Jijini Paris nchini Ufaransa.
Akizungumza wakati akitangaza kongamano hilo la kihistoria, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Liberata Mulamula, amesema ujumbe wa Tanzania kwenye kongamano hilo utaongozwa na Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango ambaye anamwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.
Amesema kongamano hilo, litajadili na kutoka na malengo ya nini kifanyike katika kuhakikisha kunakuwa na usawa wa kijinsia kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
“Wakuu wa nchi mbalimbali, taasisi, mashirika, wanaharakati wa masula ya haki na jinsia watakutana katika Jiji la Paris na kongamano hilo, linafanyika ikiwa imepita miaka 26 baada ya kufanyika Kongamano la Beijing nchini China.
“Kutakuwa na mijadala inayohusu usawa wa kijinsia katika nyanja mbalimbali. Kwa Tanzania rais wetu kwa niaba ya serikali, amechagua eneo ambalo linahusisha jinsi ya kuongeza nguvu ya wanawake katika uchumi, haki zao, kuwa na usawa wa kushiriki katika uchumi na uchumi unaozingatia haki ili kupata maendeleo.
“Kuwawezesha kumiliki ardhi, kuwawezesha kumiliki ardhi, tunajua akinamama wengi wanajihusisha na biashara ndogo ndogo, hivyo baada ya mkutano huo utakwenda kujibu masuala ya kumuwezesha mwanamke na wakati tunakwenda kwenye hilo kongamano tayari Rais Samia, alishaanza kuweka mikakati ya kuwawezesha wanawake,” amesema.
Amesisitiza kutokana na ukubwa wa kongamano hilo, rais alikuwa aende lakini kutokana na majukumu mengine ya kikazi aliyonayo amemtuma, Dkt. Mpango amuwakilishe na atakuwa na ujumbe ambao umesheheni usawa wa kijinsia hivyo akiwa huko, atawasilisha mipango ya Serikali ya awamu ya sita katika eneo hilo.
Alipoulizwa kuhusu ukatili wa kijinsia ukoje kwa Tanzania wakati wanaelekea kwenye kongamano hilo, Waziri Mulamula amesema hana takwimu rasmi lakini ukatili bado upo huku akifafanua wakati wa janga la Corona lilipoanza, shule zilifungwa na kuna taarifa ambazo zilisikika kuhusu kuongezaka kwa ukatili.
Amesema kuna mambo mengi yanayosababisha ukatili huo, ikiwemo ya mila potofu ambazo zinachochea uwepo wa ukatili unaofanywa kwa wanawake, ingawa na wanaume nao wanafanyiwa ukatili huo.
Kwa upande wake Balozi wa Ufaransa nchini, F’redric Clavier amesema amefurahishwa na Serikali ya Tanzania kutangaza kushiriki kikamilifu kwenye kongamano hilo la kizazi cha usawa.
Balozi Clavier, amesisitiza kongamano hilo la usawa wa kijinsia linakuja miaka 26 baada ya kongamano la Beijing ambalo pamoja na mafanikio yake, bado kuna changamoto ya usawa, hivyo kongamano hilo limekuja wakati muhimu na litatoka na malengo yatakayowezesha kwenda mbele zaidi.
Lengo kuu la kongamano hilo la kihistoria litaweka malengo ya kupata suluhu kutoka serikalini, taasisi, asasi, wanaharakati na watetezi wa wanawake ambapo Ufaransa itafanya kazi kwa kushirikiana na nchi mbalimbali kufikia malengo hayo.
Amesema katika kipindi cha miaka 26, kuna mafanikio mengi lakini bado hayatoshi hivyo lazima kuwepo na mipango mingine kufikia usawa wa kijinsia na kwamba vijana ndiyo wanatakiwa kuwa mstari wa mbele kwenye kuhakikisha usawa wa kijinsia unakuwepo.
More Stories
Bei za mafuta Novemba 2024,zaendelea Kushuka
TARURA yaomba Mkandarasi aitwe
Ilemela yakusanya bilioni 3.7.robo ya kwanza