December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kutoa ruzuku ya Sh.Bilioni 100 kupunguza bei za mafuta nchini

Na Nasra Bakari, TimesMajira Online

RAIS wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, ameelekeza kuwa katika kipindi hiki kabla hatujafikia mwaka mpya wa fedha serikali itoe ruzuku ya Sh.Bilioni 100 kwa ajili ya kupunguza bei za mafuta hapa nchini.

Kauli hiyo ilizungumzwa jana na Waziri wa Nishati na Madini January Makamba alipokuwa anatoa taarifa bungeni jijini Dodoma kuhusu kupanda kwa bei ya mafuta nchini alisema, Rais Samia alitoa maelekezo kwamba mwaka wa fedha ujao ni mbali kusubilia ahueni hiyo na akaelekeza kwamba ahueni itafutwe haraka zaidi katika kipindi hiki kabla hatujafika mwaka mpya wa fedha.  

Makamba alisema, serikali imeamua kutoa fedha hizo hivi sasa na ruzuku hii inatolewa kwa kupunguza matumizi ya serikali katika kipindi kilichobaki cha mwaka huu wa fedha kutolewa kwa ruzuku hii hakutagusa miradi ya maendeleo ambayo inaendelea.

“Fedha hii ya Sh.Bilioni 100 ni nafuu ya kipindi cha mpito kuelekea mwaka wa fedha ujao ambapo nafuu nyingine inayotokana na mikopo niliyoelezea hapo awali na itaelezwa kwa kina zaidi na waziri wa fedha katika bajeti ya mwaka ujao,  ruzuku hii itatolewa kwa ajili ya kupunguza bei ya mafuta kuanzia mwezi Juni mwezi huu.

“Pamoja na changamoto ya bei jambo ambalo siyo letu pekeyetu usimamizi wa sekta ya mafuta hapa nchini hasa katika kipindi hiki kigumu umekuwa wa utulivu na wa makini hii siyo kwa sababu ya magari bali ni kwa jitihada za makusudi za serikali kwa ushirikiano wa sekta binafsi”, alisema

Alisema, bei ya mafuta kupanda ni janga lakini hatari kubwa zaidi hata kwa usalama ni pale mafuta kutokupatikana sisi kama nchi hatujafikia huko kwa sababu ya jitihada za serikali.

Kwa upande wake Spika wa Bunge la Tanzania Tulia Ackson alisema, tunampongeza Rais Samia pamoja na serikali yake kwa kutueleza wabunge siku hii ya leo ndani ya muda huu mfupi za hatua mbalimbali za hapo badae  zitakazochukuliwa tunampongeza sana kwa kulisimamia jambo hili pamoja na mawazili wote kuhakikisha tunafika hapa tulipo.

Alisema wabunge nadhani nyinyi ni mashahidi kwamba jana alikuwa na kikao mpaka usiku kuhakikisha leo bunge linapewa taarifa kama ambavyo tulikuwa tumeiambia serikali kwamba tunahitaji taarifa hiyo kwahiyo ni jambo la kushukuru sana kwa hatua iliyochukuliwa.

“Kwa mujibu wa maamuzi yaliyochukuliwa sisi kama wabunge ni wajibu wetu kuwafafanulia wananchi kwamba haya tuliyoyasikia mpaka mwezi Juni siku ya bei mpya itakapotangazwa ambapo fedha hizi zilizoingizwa kama ruzuku ni wajibu wetu sisi kuchukua hatua kama serikali ilivyochukua hatua,” alisema na kuongeza

Spika wa Bunge alisema, tuendelee kujielimisha ili itakapokuja hotuba hii tuwe na mambo ya kuwapa serikali vitu vya kuyafanyia kazi maana vitu vingi tunavyoviongelea bungeni  huwa serikali inafanyia kazi.