NA Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
SERIKALI imesema itaendelea kutoa elimu kwa wadau kuhusu Sera ya Elimu na Mafunzo 2014 (Toleo la 2023) na mitaala iliyoboreshwa. Itatoa mafunzo kwa wathibiti ubora wa shule, walimu, wakufunzi, wahadhiri na maafisa elimu.
Hayo yamesema leo Mei 12,2025 Bungeni Jijini Dodoma na Waziri wa Elimu ,Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka 2025/2026 huku akisema katika kipindi hicho mapitio ya Sheria ya Elimu, Sura 353, yatakamilishwa ili kuendana na Sera mpya.
Amesema ,mapitio hayo yatahusisha pia sheria zinazohusu Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Bodi ya Huduma ya Maktaba, Baraza la Mitihani, na taasisi nyingine za elimu.
Vilevile mesema, Serikali itakamilisha zana muhimu za utekelezaji wa sera, ikiwemo Mwongozo wa Upimaji na Tathmini, Mfumo wa Taifa wa Mitaala, na miongozo ya usambazaji na upatikanaji wa walimu.
Ametaja miongozo hiyo kuwa ni pamoja na Mwongozo wa kitaifa wa kuwaendeleza kitaalamu wakufunzi na wafanyakazi wasio wakufunzi katika vyuo, mwongozo wa ushirikiano kati ya viwanda na taasisi za elimu, na mwongozo wa utambuzi wa ujuzi katika elimu ya ufundi ni miongoni mwa maandalizi yatakayofanyika.
Pia, Serikali itaandaa mwongozo wa uanzishaji wa kampuni na vituo vya ubunifu wa teknolojia (TICs) katika taasisi za elimu na utafiti, na kuhuisha miongozo ya udahili, ithibati, na elimu ya watu wazima.
Kwa mujibu wa Prof.Adolf Mkenda katika kuimarisha Mafunzo ya Amali ,Serikali itawezesha upanuzi wa shule 55 kuwa shule za sekondari za amali na pia, itaboresha miundombinu na vifaa katika vyuo vya ualimu vya Mtwara ili kufanikisha utoaji wa elimu ya amali.
Amesema,vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi vitaongezwa hadi 504, huku 898 vikiwa vya mafunzo ya ufundi stadi. Serikali itasajili shule 100 za sekondari za ufundi na kudahili wanafunzi 265,000 wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi.
Katika juhudi za kuboresha mazingira ya kujifunzia amesema Serikali itajenga awamu ya pili ya vyuo 64 vya VETA vya wilaya na chuo kimoja cha Mkoa wa Songwe. Pia, ujenzi wa vyuo vipya vitano katika mikoa ya Rukwa, Kigoma, Mtwara, Morogoro na Zanzibar utaanza.
Vile vile amesema ,ujenzi wa mabweni, maktaba, karakana na nyumba za watumishi katika vyuo mbalimbali kama vile Dodoma na Arusha pia utaendelea.
More Stories
Wanawake watakiwa kutochafuana kuelekea uchaguzi mkuu
Serikali Kuboresha Elimu ya Ufundi: Shule 55 Kubadilishwa Kuwa Sekondari za Amali
Waliopata ufaulu wa juu kidato Cha sita mchepuo wa sayansi kupata ufadhili