Na Mwandishi Wetu, TimesMajira online
SERIKALI imewahakikishia Chama cha Wamiliki wa Mabasi hapa nchini (TABOA) kuwa itahakikisha inatatua na kumaliza changamoto zote ambazo ni kikwazo kwa wafanyabiashara hao ikiwamo mfumo mpya wa ukatishaji tiketi mtandao.
Huku ikizitaka taasisi zinazosimamia usafirishaji kuhakikisha wanatatua kero na malalamiko yanayohusu wasafirishaji kwa wakati pindi zinapofika ofisini kwao.
Hayo yamebainishwa jijini Dodoma na Naibu Waziri wa uchukuzi Mwita Waitara alipokutana na TABOA kwa lengo kusikiliza kero mbalimbali zinazowakumba katika biashara zao.
Amesema Serikali ina nia nzuri ya kuhakikisha wafanyabiashara wa mabasi wanafanyakazi bila ya kuwa na vikwazo kwani wao ni moja ya sekta muhimu ya kuchocheo uchumi hapa nchini.
“Serikali inania nzuri sana na lengo lake ni kuhakikisha ninyi mnafanyakazi kwa uhuru ndio maana leo nimekuja hapa niwasikilize nini kikwazo kwenu kwa kuwa sekta yenu ni muhimu sana kuwasafirisha wananchi ili nao walipe kodi nchi ijiendeshe” amesema Waitara.
Ameongeza kuwa “Nimewasikiliza kero zenu zote niwahakikishie tu kero zenu zote zitafanyiwa kazi hata hii kelele ya muda mrefu ya tiketi mtandao tutalifanyia kazi kwa kuwa taarifa ni kwamba mfumo unafanyiwa marekebisho bado haujawa rasmi utaboreshwa” amesema.
Ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA) kuhakikisha kero, changamoto na malalamiko mbalimbali ya TABOA yanafanyiwa kazi haraka pia wajenge utaratibu wa kusikiliza kero na kuzijibu kwa wakati ili sekta ya usafirishaji iweze kukua hapa nchini.
“Nimepata ushahidi hapa kwa barua mbalimbali kutokujibiwa na mimi mwenyewe shahidi kuna taarifa yangu niliomba haijafanyiwa kazi pia kuna mbunge mwenzangu katuma maombi ya kubadilisha tu rout(njia) lakini mpaka leo haijajibiwa shida ni nini” amesema.
Aidha Waitara amesema atahakikisha anawakutanisha LATRA na TABOA ili malalamiko yao yote yaweze kujibiwa moja kwa moja ili changamoto hizo ziweze kuondoka kabisa sambamba na hilo ili LATRA waweze kuwapitisha katika mfumo huo ili TABOA waweze kuelewa namna mfumo huo unavyofanyakazi na malengo ya kuanzishwa kwake.
Awali wajumbe wa TABOA wameiomba serikali kuitazama upya LATRA na muundo wake kwani kanuni zao nyingi si rafiki kwao zinaweza kupelekea kupoteza mitaji yao kwa kufilisika kutokana na makato mengi katika biashara hiyo.
Pia wamesema mfumo wa tiketi mtandao wao ndio waanzilishi lakini sasa imekuwa tofauti na malengo ya kuanzishwa kwake kwa sasa imekuwa mwiba kwao hasa baada ya kutakiwa kujaza flot kabla ya kuanza kufanyakazi na kuwa na utitili wa makato tofauti na mashine nyingine za kutolea lisiti.
More Stories
Makalla:Kupanga fujo ni dalili za kushindwa uchaguzi
Tanzania yapanda viwango Utawala wa Sheria Duniani
Rais Samia apeleka neema Tabora