Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
CHAMA cha wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU) Taifa kimetaja kero saba ambazo chama kinakabiliana nazo huku wakiamini serikali itazishughulikia
Kero hizo zimetajwa jijini hapa leo Januari 14,2026 na Katibu Mkuu TALGWU-Taifa Wandiba Ngocho wakati akisoma risala kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Ajira na Mahusiano,Deus Sangu wakati wa Ufunguzi wa kikao cha 31 cha Baraza kuu la TALGWU Taifa kilichofanyika jijini Dodoma amesema kuwa chama hicho pamoja na kutendewa mambo makubwa na mazuri lakini bado kinakabiliwa na changamoto kadhaa.

Ngocho amezitaja changamoto hizo zinazowakabili watumishi kuwa ni pamoja na Kutolipwa kwa wakati fedha za likizo kwa Wanachama wa chama hicho.
Amesema kuwa kuna changamoto kubwa katika utaratibu wa malipo ya fedha za likizo kwa Watumishi waliopo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.
“Hii inatokana na utaratibu uliopo kwa watumishi hawa kulipwa likizo kupitia fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri.
“Ieleweke kwamba Halmashauri nyingi nchini hushindwa kufikia malengo ya mapato ya ndani kutokana na vyanzo vichache vya kukusanya mapato.

“Suala hili linasikitisha sana kwani wapo watumishi ambao hawajalipwa stahiki zao za likizo tangu mwaka 2018 na hali hii ikiongezeka mwaka hadi mwaka. Ili kutimiza takwa hili la kisheria la malipo ya likizo, tunaiomba Serikali itenge bajeti ya fedha kutoka mfuko mkuu wa Serikali na sio kutegemea mapato ya ndani ya Halmashauri kama inavyofanyika kwa Watumishi wa kada ya Ualimu”ameeleza.
Changamoto nyingine aliyoitaja ni pamoja Malipo ya leseni ya kutoa huduma kwa Watumishi wa kada ya Afya (practice license).
” Mheshimiwa Waziri, kuna manung’uniko na malalamiko makubwa kwa Watumishi wa Kada ya Afya hususan madaktari, wauguzi, wafamasia, wataalamu wa maabara, wataalamu wa mionzi na wafiziotherapia ambao watakiwa kujilipia ada ya leseni ya kila mwaka huku wakiwa wanatekeleza majukumu ya kutoa huduma kwa umma.
“Iwapo watashindwa kulipa ada hiyo wanakosa haki ya kupandishwa madaraja na kushindwa kubadilishwa vyeo.
“Naomba ieleweke kwamba wengi wa watumishi hawa hawafanyi biashara kwa leseni hizo bali kuwahudumia wananchi kwa maendeleo ya Taifa letu kuhusu suala hili, tunaiomba Serikali kufanya yafuatayo.

“Waajiri kuwalipia Watumishi wa kada ya Afya ada hizo kwa kuwa wanatumia taaluma zao kuwahudumia wananchi na si kufanya biashara.
“Leseni ya kutoa huduma (practice license) isiwe sehemu ya kigezo cha Watumishi wa kada ya Afya kupandishwa madaraja katika Utumishi wa Umma.
“Kuibuka upya kwa baadhi ya Viongozi wa kisiasa kuwadhalilisha Watumishi wa Umma Mheshimiwa Waziri, tumeanza kushuhudia siku za hivi karibuni imeanza kuibuka upya kwa tabia ya baadhi ya viongozi wa kisiasa kuwadhalilisha Watumishi wa Ummawanapotekeleza majukumu yao, hususan wakati wa ziara za ukaguzi wa miradi ya maendeleo zinazoambatana na vyombo vya habari.
“Ingawa TALGWU inaunga mkono kikamilifu usimamizi na uwajibikaji mahala pa kazi, lakini Chama kinaona kuwa si sahihi, haki wala maadili kwa viongozi kutoa matamko ya kuwatuhumu Watumishi wa Umma hadharani kwa kuwaita wezi au wazembe wakati tuhuma hizo bado hazijachunguzwa wala kuthibitishwa na mamlaka husika. Vitendo hivi vinadhalilisha Watumishi wa Umma, vinashusha morali ya kazi, na kusababisha wananchi kukosa imani kwa Utumishi wa Umma na taasisi za Serikali kwa ujumla.
“TALGWU inasisitiza umuhimu wa Viongozi wa kisiasa kufuata taratibu za kisheria na kiutawala pale changamoto zinapojitokeza, na tunatoa wito kwa viongozi wa kisiasa kuzingatia misingi ya heshima, haki na ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yao kwani TALGWU tunawajibu wa kusimama imara katika kulinda heshima, haki na hadhi ya Watumishi wa Umma kwa maslahi ya Taifa.”ameelezea Kaimu Katibu Mkuu TALGWU Taifa.

Changamoto nyingine ya nne aliyoitaja ni watumishi wa Serikali kutolipwa kwa wakati fedha za uhamisho.
Amesema kuwa bado kuna malalamiko makubwa kwa baadhi ya Waajiri katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kuwahamisha Watumishi bila kulipa stahiki za uhamisho ingawa Serikali ilishatoa maelekezo kwa Waajiri kutowahamisha Wafanyakazi bila kuwa na bajeti.
“Hivyo tunaiomba Serikali kuwakumbusha Waajiri nchini kulipa stahiki hii kwa Watumishi kwa mujibu wa sheria.
Ameitaja changamoto ya tano kuwa ni kuwepo kwa Changamoto ya mfumo wa upimaji wa utendaji kazi kwa Watumishi wa Umma(PEPMIS).
“TALGWU tunatambua jitihada za Serikali katika kuboresha na kuwezesha matumizi sahihi ya mfumo wa upimaji wa utendaji kazi kwa Watumishi wa UmmaambaoMtumishi anajihudumia mwenyewe kwa njia ya mtandao isipokuwa bado kuna uhitaji mkubwa kwa upande wa elimu ya matumizi sahihi ya mfumo huo.
“Hivyo tunaiomba Serikali iendelee kutoa elimu ya kutosha juu ya matumizi ya mfumo huo kwa Wafanyakazi na wasimamizi wao wa karibu (immediate supervisors)”ameeleza.
Akiendelea kusoma risala Ngocho ameeleza kuwepo na Changamoto katika miundo ya utumishi hasa katika kubadilishiwa vyeo (Recategorization).
Ameeleza kuwa kuna changamoto kubwa katika miundo ya Utumishi kwa kada zisizo za walimu mfano Maendeleo ya Jamii, Afya, Kilimo, Ardhi, Utumishi na Utawala pamoja na Uhasibu kubadilishwa kada pindi wanapotoka masomoni.
Amesema kuwa Miundo inawalazimu kupelekwa katika cheo cha chini cha kuanzia bila kuzingatia uzoefu katika Utumishi wa Umma.
“Hivyo, tunaiomba Serikali ipitie upya na ibadilishe utaratibu na kuzingatia uzoefu katika kushughulikia suala hili.
“Aidha, kwa upande wa kupandishwa cheo Chama kinashauri na kuiomba Serikali kwamba sharti la kigezo cha shahada ya uzamili liwe ni kigezo cha nafasi za uteuzi badala ya kuwa sharti la kimuundo”ameeleza.
Changamoto ya saba aliyoisoma kwenye risala yake Ngocho ni pamoja na kutokuhuisha kwa wakati Mabaraza ya Wafanyakazi.
“Bado kuna baadhi ya Halmashauri hazifanyi vikao vya mabaraza ya Wafanyakazi kwa mujibu wa sheria pamoja na mabaraza mengi yalioisha muda wake kutohuishwa.
“Mpaka kufikia Desemba 2025 kati ya Mabaraza 197 (184 ya Halmashauri na Mabaraza 13 ya Wizara tunayoshiriki kama Chama) ni Mabaraza 137 tu ndiyo yapo hai na Mabaraza 60 yameisha muda wake.
“Hivyo tunakuomba Mhe. Waziri uwaelekeze Waajiri ambao bado hawajahuisha Mabaraza ya Wafanyakazi kutekeleza matakwa ya kisheria”ameeleza Ngocho.
Akijibu utatuzi wa kero hizo Waziri Sangu amesema kuwa wakikutana kwenye kikao ambacho kitajumuisha wafanyakazi,Waajiri na Serikali kikao ambacho amekiita ni cha ,’UTATU’amesema ajenda moja ya ajenda kubwa za kikao hicho zitakuwa ni kero zilizotajwa kwenye kikao hicho cha 31 cha Baraza la TALGWU.

Sangu amesema kuwa changamoto nyingi walizozitoa kwenye kikao hicho alishawahi kuzifanyiakazi akiwa Naibu Waziria ambapo amesema alitembea Mikoani kote na aligundua matatizo ya wafanyakazi yanaendana na kujirudia.
“Na hapa ndiyo tunasema serikali kuna jambo inapaswa kufanya ni kweli imekuwa ni malalamiko ya muda mrefu ya kutolipwa malipo ya likizo kwa wanachama wa TALGWU na vyama vingine.
Aidha amesema kuwa jambo la malipo ya likizo lilitolewa maelekezo na Katibu Mkuu Utumishi 2025 na kubainishwa kuwa tatizo hilo ni kubwa.Ambapo alitoa maelekezo na alitoa waraka kwa waajiri wote serikali za mitaa na pahala pengine kuhakikisha kwamba unapokuwa na mtumishi ujue mtumishi ataenda likizo na unapopanga bajeti yako mpangie bajeti yake inayohusiana na rikizo.
“Sasa jambo hili naomba niwatoe shaka na mimi nitakuwa hamasa nalibeba kwa uzito mkubwa kuhakikisha waraka ule uliotolewa na Katibu Mkuu Utumishi kwa waajiri unasimamiwa na wale ambao wanamalimbikizo yao yanashughuliwa”.amesema.
Pamoja na hayo Sangu amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita inawatambua na kuwathamini kwa kazi kubwa inayofanywa na chama hicho kwasababu bila wao mipango ya maendeleo ya taifa isingewea kuongezeka kwa ufanisi mkubwa.
Amesema kwa kutambua umuhimu wa wananchi na wafanyakazi Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ameendelea kuweka mazingira wezeshi kwa watumishi na wafanyakazi na kuboresha maslahi yao kwa vitendo.
“Kwa kipindi kifupi cha Uongozi Rais wa Samia serikali imeongeza ajira kabla ya uchaguzi iliajiri watumishi zaidi ya 140,000 na mpaka Januari 12 ,Rais ameongeza ajira 22,000 za Afya na Elimu .
“Kusipokuwa na ajira hata vyama vya wafanyakazi vinaathirika kwasababu ili vyama vya wafanyakazi viendelee lazima viwe na wafanyakazi kwasababu ili kuviendesha wanahitaji michango ya wanachama.

More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi