October 27, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kupeleka umeme vitongoji vyote Igalula

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira

SERIKALI kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeendelea kutekeleza miradi ya kusambaza umeme katika Jimbo la Igalula mkoani Tabora, ikiwa na lengo la kuhakikisha vitongoji vyote ambavyo bado havijafikiwa na huduma hiyo vinapatiwa umeme ifikapo mwaka 2030.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Nishati,Salome Makamba, wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Igalula,Juma Mustafa Kawamba, aliyetaka kujua ni lini Serikali itafikisha umeme katika vijiji na vitongoji vya jimbo hilo ambavyo bado havina huduma hiyo.

Salome amesema kuwa hadi kufikia Oktoba 2026, vijiji vyote 58 vya Jimbo la Igalula vimefikishiwa miundombinu ya umeme, huku vitongoji 87 kati ya 275, sawa na asilimia 31.64, vikiwa vimefikiwa na huduma hiyo.

Amefafanua kuwa kwa sasa wakandarasi wanaendelea na utekelezaji wa Mradi wa Kupeleka Umeme Vitongojini Awamu ya Pili A na B (HEP IIA na HEP IIB), unaohusisha vitongoji 48 vya jimbo hilo, vikiwemo Miyenze, Majimaji, Igembensabo na Migusa vilivyopo katika Kijiji cha Miyenze, Kata ya Miyenze.

Aidha,Salome amesema Serikali kupitia REA inaendelea na maandalizi ya Mradi wa Universal Hamlet Electrification and Last Milestone Connectivity Project, unaolenga kufikisha huduma ya umeme katika vitongoji vyote vilivyosalia nchini ifikapo mwaka 2030.

Amesisitiza kuwa utekelezaji wa mradi huo utawezesha vitongoji vyote vya Jimbo la Igalula ambavyo bado havijafikiwa na huduma ya umeme kunufaika na nishati hiyo ifikapo mwaka 2030.