May 30, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kupeleka Mwalimu wa Kilimo Masoka sekondari

Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online – Dodoma

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Zainabu Katimba, amesema kuwa Serikali itafanya jitihada za kuhakikisha inapeleka mwalimu wa somo la Kilimo katika Shule ya Sekondari Masoka iliyopo katika Jimbo la Moshi Vijijini, mkoani Kilimanjaro.

Katimba alitoa kauli hiyo leo, Mei 28, 2025, bungeni jijini Dodoma, kufuatia swali la Mbunge wa Moshi Vijijini, Profesa Patrick Ndakidemi, ambaye alitaka kufahamu mpango wa Serikali kuhusu upelekwaji wa mwalimu wa somo la Kilimo katika shule hiyo.

“Shule ya Sekondari Masoka iliyopo katika Jimbo la Moshi Vijijini ni ya mchepuo wa Kilimo, lakini haina mwalimu wa kufundisha somo hilo. Je, Serikali ina mkakati gani wa kusaidia kupeleka walimu wa somo hilo katika shule hiyo?” amehoji Prof. Ndakidemi.

Akijibu swali hilo, Katimba alitumia fursa hiyo kumhakikishia Mbunge huyo kuwa Serikali itayafanyia kazi maombi hayo mahsusi ili kuhakikisha kuwa mwalimu wa somo la Kilimo anapelekwa shuleni hapo na wanafunzi wanapata fursa ya kujifunza somo hilo muhimu.

“Profesa Ndakidemi amekuwa akifanya ufuatiliaji wa hali ya juu wa masuala mbalimbali katika jimbo lake, na namfahamu kuwa ni mdau mkubwa sana wa kilimo hapa nchini. Kwa hiyo, hili tutalitekeleza,” alisisitiza Naibu Waziri huyo

Wakati huo huo Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Maryprisca Mahundi amempongeza Mbunge Ndakidemi kwa ufuatiliaji miradi ya maji huku lakini pia kwa kusihuru Serikali kwa kile inachofanya katika utekelezaji wa miradi mbalimbali

Awali Prof.Ndakidemi ameishukuru Serikali kwa kupeleka zaidi ya shilingi milioni 800 kufanya ukarabati wa miundombinu ya maji katika kata ya Old Moshi Mashariki .

Amesema tayari ameshaiomba Serikali ipeleke fedha kwa ajili ya kumalizia usambazaji wa mabomba katika kata hiyo na katika Bajeti ya mwaka huu Jimbo lake limepewa pesa .