December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kulipa madeni ya vyombo vya habari

*Ni zaidi ya bil. 18/- Waziri Nape asema nia yao sio kuvifanya vyombo vya habari vishindwe kufanyakazi, asisitiza dhamira ya Rais Samia, Biteko atia neno

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline, Dodoma

SERIKALI imeanza kufanya mipango ya kufanya utekelezaji wa kulipa vyombo vya habari, ambapo hadi sasa vinadai Serikali zaidi ya sh. bilioni 18 na kati ya hizo gazeti la Serikali linaongozwa kwa kudai zaidi ya bilioni 10.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, wakati akizungumza kabla ya kumkaribiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Dotto Biteko, kufungua mkutano wa kitaaluma wa 13 wa mwaka wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) ulioanza jana jijiji Dodoma.

Amesema taarifa ya uchumi kuhusu vyombo vya habari imekamilika ni nzuri sana ina mambo mengi sana yameingizwa humo ndani. “Na kama mnavyojua maagizo ya jambo hili yalitolewa na Rais, kwa hiyo lazima tuwasilishe kwake, tunasubiri ratiba yake tutaiwasilisha hivi karibuni,” amesema Nape.

Waziri Nape amesema kati ya zaidi ya sh. bilioni 18 ambazo vyombo vya habari vinadai, kiasi cha sh. bilioni 5 zinadaiwa kutoka kwenye halmashauri, ambazo inavyoonekana hawapunguzi wala hawatikisiki chochote, jambo ambalo sio sawa.

Aidha, Nape amesema kiasi kingine cha pesa kilichobaki kinadaiwa na taasisi za Serikali. “Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu naomba niseme hapa, sidhani kama hawa walikuwa wanatagaza bila kuwa na bajeti.

Nataka kuamini kuwa kuna kauzembe fulani na wanaliona hili jambo sio tatizo kubwa na kwa sababu kaka yangu wewe ndiye Naibu Waziri Mkuu tena anayeshughulikia Uratibu wa Serikali, nina hakika tukiamua kubana kidogo katika bajeti tunazoendelea nazo tunaweza kulipa.

Halmashauri na taasisi za Serikali zitenge fedha zianze kulilipa hili deni itatusaidia kutoka hapa tulipo .Ukisoma ile ripoti pamoja na mapendekeo mengi kuna hili la deni la Serikali, ndiyo maana hapa Balile (Mwenyekiti wa TEF) amesema na ametumia mfano wa duniani,” amesema Nape na kuongeza;

“Nia yetu kwa kweli sio kuvifanya vyombo vya habari vishindwe kufanyakazi, lakini nadhani tukaze kidogo ili haya madeni yaanze kulipwa. Waziri Mkuu aliagiza yaanze kulipwa, Rais aliagiza yaanze kulipwa, lakini nadhani iko haja…

Naibu Waziri Mkuu (Biteko) ebu viokoe vyombo vya habari hali sio sawa, Balile hakutaja hapa, New Habari wamefunga na walikuwa na mtambo mzuri kabisa, mimi kama waziri wenu sitaki kumung’unya maneno Serikali lazima wajipange kulipa madeni wanayodaiwa ya vyombo vya habari, vinginevyo tutaua vyombo vya habari.

Kama ambavyo tunalipana posho, kama ambavyo tunalipana mishahara, vivyo hivyo tulipe vyombo vya habari na wao wakalipe mishahara wafanyakazi wao. Tukifanya hivyo, mambo yatakwenda.”

Amesema hilo la kutenga fedha kwenye bajeti wao kama wizara hawana tatizo nalo ni jambo ambalo wanaweza wakazungumza wakajipanga, sasa iwe bilioni moja, hana uhakika anaamini sio jambo kubwa.

***Kauli ya Biteko

Akizungumzia hilo, amesema atamwomba Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na viongozi wakuu wa Serikali wazisihi Wizara na Taasisi za Umma zitenge bajeti ya kutosha kulipia gharama za matangazo pindi wanapotumia huduma hii kwa vyombo vya habari.

“Nafahamu kuwa bila matangazo, redio, televisheni, magazeti na mitandao ya kijamii inakuwa na kazi ngumu kuendelea kutoa huduma hii ya habari. Kiuhalisia habari ni huduma si biashara.

Hakuna uwezekano wa kutengeneza faida kupitia vyombo vya habari, hivyo inabidi vyombo vya habari viwezeshwe kwa njia ya matangazo navyo vitusaidie kufikisha ujumbe kwa kwa wananchi tujenge taifa imara,” amesema.

***Ushirikiano

Wakati huo huo, Nape alipongeza ushirikiano ambao anapata kutoka kwa wanahaari ikilinganishwa na kipindi cha nyuma alichokuwa waziri wa habari. Amesema ushirikiano wa wanahabari ni mkubwa na ushahidi upo, ikiwemo walivyoshiriki Maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano.

Alisema hata wakati Rais Samia anaadhimisha miaka mitatu ya uongozi wake, wanahabari walifanyakazi kubwa, makongamano mengi yalifanywa na wanahabari pamoja na hali yao ngumu ya kiuchumi.

Amesema uwepo wao hapo ni matokeo ya ushirikiano. Alisema Mwenyekiti wa TEF, amekiri kuwa katika eneo la Uhuru wa vyombo vya habari mambo yanaenda vizuri. Amesema kwa sasa wanahabari wanaandika habari bila hofu na kama ipo, pengine ni kwa sababu ya mazingira ambayo tumetoka nayo.

“wakati mwingine, imeshatokea kwenye vyombo vya habari, watu waanakaa wanatishana wenyewe, wanasema kuna maagizo kutoka juu, ukiwauliza hayo maagizo yametoka wapi, wanasema hapana, tumeona hilo jambo halijakaa sawa,” amesema Nape.

Amesema wameambiwa wanahari watimize wajibu wao kwa kuzingatia sheria, taratibu, lakini kikubwa busara, kwani nchi ni yao.”Wakati fulani jambo fulani linaweza kuwa la kweli, lakini ukilisema katika mazingira fulani hayatajenga, hiyo ni busara ya kawaida, mtu kamtukana baba yako, kweli ni habari, ukiandika hiyo ni shauri yako mwenyewe,” amelisema.

Amesema hilo halikuja kwa bahati mbaya bali ni uamuzi wa dhati alioufanya Rais Samia wa kuamua makusudi vyombo vya habari viwe huru ili vitoe mchango mkubwa katika kukuza utawala bora na utawala wa sheria nchini.

“Sisi Serikali tutaendelea kusimamia hili ili kuhakikisha wanaandishi wa habari na vyombo vyao vinafanyakazi zao kwa utulivu, bila kubugudhiwa ili mradi havivunji sheria na taratibu ambazo tumejiwekea,” amesema.