December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kujenga shule za sekondari za kata 226

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

SERIKALI imesema katika kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia katika ngazi ya elimu ya msingi, sekondari na ualimu,itawezesha ujenzi wa shule za sekondari za kata 226, nyumba za walimu 184 wa sekondari na ununuzi wa vifaa vya maabara.

Hayo yamesemwa jijjki hapa leo Mei 7,2024 Bungeni na Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Waziri Prof.Adolf Mkenda wakati akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Bajeti ya Wizara hiyo.

Ambapo amesema serikali itawezesha ujenzi wa madarasa 2,018 (msingi 1,221 na sekondari 797),mabweni 114 kwa shule za sekondari,nyumba za walimu 658 (msingi 567 na sekondari 81) matundu ya vyoo 2,848 (msingi 1,514 na sekondari 884), maabara 10 na vituo vya walimu (TRCs) 300 kwa lengo la kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.

Aidha,amesema itakamilisha ujenzi vyumba vya madarasa 111 katika shule za msingi 37, matundu ya vyoo, maabara, nyumba za walimu na mabweni katika shule za sekondari 50 na itaweka nishati safi ya kupikia ili kuendelea kuhifadhi na kuimarisha mazingira katika vyuo vya ualimu 11 (Nachingwea, Katoke, Kleruu, Tabora, Dakawa, Patandi, Mpwapwa, Sumbawanga, Mhonda, Kasulu na Monduli).

Vilevile, itanunua samani kwa ajili ya Chuo cha Ualimu Sumbawanga, Mhonda, Dakawa na Ngorongoro.