Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
NAIBU Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Pauline Gekul amesema Serikali itaendelea kuipa kipaumbele michezo ambayo inafanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.
Gekul ametoa kauli hiyo alipotembelea kambi ya timu ya Taifa ya mchezo wa Kabaddi katika shule ya Sekondari Nguva iliyopo Wilayani Kigamboni Jijini Dar es Salaam ambayo inajiandaa na mashindano ya Kabaddi ya Afrika yatakayoanza kutimua vumbi Juni 29 hadi Julai 5, 2021 katika viwanja vya Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam.
Katika mashindano hayo ya Afrika, nchi zilizothibitisha kushiriki ni Kenya, Cameroon, Misri, Zimbambwe, Mauritania pamoja na Algeria ambao bado hawajataja idadi ya timu zitakazokuj huku Nigeria na Tunisia zenyewe zitatoa wawakilishi wao kuja kushuhudia mashindano hayo kwakuwa timu zao hazitashiriki.
Lakini pia Kenya italeta timu ya Circle Kabaddi ambayo itachuana na timu ya Magereza kutokana hapa nchini ambapo mchezo huo hautakuwa sehemu ya mashindano bali utachezwa katika mashindano kama sehemu ya onyesho.
Amesema, wao kama serikali wataendelea kushirikiana bega kwa bega na timu hizo ikiwemo hiyo ya Kabaddi huku akiwapongeza wadhamini waliojitokeza kudhamini kambi hiyo na kuwataka viongozi wa Kabaddi kushirikisha sekta nyingine ikiwemo Wizara ya Maliasili na Utalii kwa ajili ya kutangaza vivutio vilivyopo nchini katika mashindano hayo.
“Niombe pia mjaribu kuzishirikisha sekta nyingine katika fursa hii muhimu, mfano ndugu zetu wa Utalii ambao wanaweza kutumia hii nafasi iliyopo kutangaza vivutio vya Utalii vilivyopo nchini kwa mataifa ambayo yanakuja kushiriki mashindano haya,” amesema Gekul.
Pia amewataka wachezaji waliopo kambini kufanya mazoezi kwa bidii kwa siku zilizobaki ili kuhakikisha wanalibakisha kombe la Afrika nyumbani kama mwenyeji wa mashindano ya mchezo wa kabaddi Afrika.
“Itakuwa vizuri kama tutajituma mazoezini ili tuweze kuchukua ubingwa kwa mashindano haya. Sisi kama wenyeji, itakuwa ni aibu sana kama tutatolewa mapema hivyo ni lazima tukapambane ili tuweze kuliwakilisha vyema Taifa letu,” amesema Gekul.
Kuelekea katika mashindano hayo, timu kutoka nje ya nchi zinatarajiwa kuwasili hapa nchini Juni 28 tayari kwa ajili ya mashindano hayo huku Tanzania wakitamba kupambana kufa na kupona kuhakikisha kombe hilo linabaki hapa nchini.
Mwenyekiti wa Chama cha Mchezo wa Kabaddi Tanzania (TKSA), Abdallah Nyoni amesema, kikosi chao kinaendelea vizuri jambo linalowafanya kutokuwa na wasiwasi wowote kuelekea kwenye mashindano hayo.
Amesema, kwakuwa Tanzania ni mwenyeji basi watahakikisha wanapambana kufa na kupona ili kuweza kufanya vizuri na kuubakiza ubingwa huo hapa nchini jambo litakalosaidia kuitangaza zaidi nchi kimataifa kupitia mchezo huo.
“Tunalishukuru Shirikisho la Kabaddi Afrika kwa kuipa nafasi Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano haya jambo ambalo litachangia kukuza mchezo huu hapa nchini pamoja na kupata fursa ya kuutangaza utalii wetu Kimataifa kwani ni mchezo mkubwa unaotambulika zaidi katika bara la Asia,” amesema Nyoni.
More Stories
Zanzibar kuzalisha wachezaji wenye vipaji
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes
Rais Samia: Yanga endeleeni kuipeperusha bendera ya Tanzania