April 3, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kuhakikisha wananchi wanaboresha taarifa zao

Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza

Serikali imewaondoa hofu wananchi ambao bado hawajaboresha taarifa zao katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, kwani inaendelea kufanya juhudi za kuhakikisha kila mmoja anafikiwa kwa wakati,ili kila mmoja aweze kupata fursa ya kushiriki katika uchaguzi mkuu mwaka huu.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwafnza, Said Mtanda,wakati akizungumza na waumini wa dini ya Kiislamu katika Baraza la Idd lililofanyika jijini Mwanza.

 Sanjari na hayo Mtanda amewashukuru wananchi wa Mwanza kudumisha amani na utulivu mkoani humo huku akisisitiza kuwa amani ni muhimu kwa ustawi wa taifa,haichagui dini, kabila, rangi, wala hali ya kiuchumi, amani ni kama yai; likivunjika, halirekebishwi tena.

Aidha, amesema,malezi bora ni haki ya kila mtoto, wazazi wanapaswa kuwalea kwa kuzingatia imani ya dini na maadili ya taifa.Hivyo amewahimiza wazazi kuwalea watoto wao kwa upendo na kuzingatia haki zao pamoja na kuwalinda dhidi ya ukatili wa aina yoyote.

Pia amesema, wazazi wanapaswa kuandika wosia na mirathi, ili kupunguza migogoro katika familia baada ya kifo,kufanya hivyo ni kuimarisha amani na utulivu katika familia na jamii kwa ujumla.

Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hassan Kabeke,amesisitiza umuhimu wa amani katika taifa , akisema kuwa Baraza la Idd ni fursa nzuri kwa serikali kuzungumza na Waislamu baada ya mwezi wa Ramadhani ambapo  BAKWATA imejizatiti kujenga vituo vya afya saba mkoani humu, hivyo kusaidia juhudi za serikali katika kuboresha huduma za afya.

Katibu Mwenza wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini, Askofu Robert Bundala, amesisitiza umuhimu wa umoja na amani, akisema Wakristo na Waislamu wanapaswa kushikamana na kuendelea kulinda amani ya nchi yetu, ni mali adhimu, ambayo ni rahisi kupoteza lakini ni ngumu kuipata tena.

“Katika uchaguzi huu, tusijiingize katika matabaka ya kidini au kikabila. Kila mtu anapaswa kuchagua kiongozi bora kwa maslahi ya taifa letu, na tuendelee kuishi kama wamoja,” amesema Bundala.

Sheikh Baruti wa Istiqama amesisitiza kuwa vijana ni nguzo muhimu ya taifa na wanapaswa kutambua wajibu wao katika kulinda amani huku akiwahimiza  kuchukua nafasi yao katika kulinda amani wakati wa uchaguzi mkuu na kuepuka kujihusisha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani.

Kwa upande wake, Abuu Maftaha wa Buhongwa Islamic ametoa wito wa kuendelea kujenga vituo vya afya na kutoa huduma bora kwa wananchi, kwamba kujenga vituo hivyo, wananchi wataweza kupata huduma bora za afya, huku akimpongeza Sheikh Kabeke kwa juhudi za kuendeleza miradi hiyo ya afya.

Show quoted text