November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kuhakikisha mbegu za asili zinatambulika katika mfumo rasmi wa kisheria na kisera

Na David John timesmajira online

WIZARA ya Kilimo nchni imesema ili kuhakikisha mbegu za asili hazitoweki, serikali itahakikisha zinatambulika katika mfumo rasmi wa kisheria na kisera, na kuongeza msukumo kwa vituo vya kuzalisha mbegu hizo.

Ufafanuzi huo umetolewa hivi karibuni na Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe wakati akijibu swali, kuhusu ni mikakati gani ambayo Serikali kupitia wizara hiyo inayo kuhakikisha mbegu asili hazipotei.

Bashe, kwaza amekiri wakulima nchini kutumia mbegu asili lakini ni wazi kuwa mbegu hizo hazipo kwenye mfumo rasmi jambo ambalo linaweza kupelekea kupotea Kwa mbegu hizo.

Amefafanua Kuwa mikakati ya serikali ni kuhakikisha mbegu hizo zinakuwa kwenye mfumo rasmi ambao utawezesha kupatikana katika masoko mbalimbali ya mbegu, hivyo wakulima wengi watazipata na kufaidika nazi.

“Niseme tu hakuna shaka kuwa kwa mujibu wa sera na sheria yetu ya mbegu ya 2003 mbegu zinazotambulika kwenye mfumo ni zile za madukani, hizi za asili ambazo zipo kwa wakulima moja kwa moja zinatumika ila sio rasmi.”amesema Bashe

Nakuongeza Kuwa “Mimi naamini kutokana na kasi ya dunia kuhitaji vyakula vilivyolimwa kwa mbegu asili, hatuna budi kuongeza nguvu kwenye eneo hilo ili ziwe endelevu kwa vizazi vijavyo,” amesisitiza

Ameongeza Kuwa wao kama wizara wahatakikisha kuwa mbegu hizo zinakusanywa na kuandaliwa katika mazingira ambayo uasili wake utaendelea na ubora ubaki palepale.

Pia Bashe amewataka wakulima kuendelea kutumia mbegu asili kwa kuwa mazao yake yana uhakika wa soko duniani kote, na kuwasisitiza kutunza katika mazingira rafiki, ili ziwe salama kwa afya za walaji.

Amesema wizara itaendelea kushirikiana na taasisi zake za kilimo na wadau mbalimbali kuhakikisha tafiti zinafanyika katika eneo hilo la mbegu asili ambazo ni muhimu kwa afya, uchumi na maendeleo endelevu.

“ Hapa nasisitiza kuwa sisi kama wizara hatujakataza kilimo cha mbegu asili, uzuri ni kwamba mimi mwenyewe natumia mbegu asili najua faida yake, hivyo nitapambana kwa kila njia kuhakikisha mbegu hizi zinalindwa, na kutuzwa” amesema.

Kwaupande wake Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Mashiriki yasiyo ya Kiserikali yanayohamasisha utunzaji wa Baionoai ya Kilimo Tanzania (TABIO), Addallah Mkindi, amesema Serikali inapaswa kuweka mkazo katika kilimo kinachotokana na mbegu asili kwa kwani kina faida na ni salama kwa afya za watumiaji.

Mkindi ameongeza Kuwa takwimu zinaonesha asilimia 70 ya wakulima ambao wamelima zaidi ya hekta milioni 13 nchini wanatumia mbegu asili, hivyo ni wazi mbegu asili ndio uti wa kilimo nchini.

“kuna tatizo la mbegu asili kutotambulika rasmi kisheria na kisera,hapa nchini kwetu lakini ndio zimeshika asilimia 70 ya kilimo, hivyo Serikali iweze kusimamia eneo hili kama ambavyo imekuwa ikifanya kwani lina umuhimu kwa binadamu,” amesema.

Kiongozi huyo amesema wao kama wadau wa mbegu asili wataendelea kutoa elimu kwa wakulima kuendeleza kilimo cha mbegu asili kwa kuwa kina faida nyingi na tija kubwa kuliko watu wanavyodhani.