Veronica Simba – Biharamulo
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani ameuagiza uongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kuhakikisha kuwa, ifikapo mwishoni mwa mwezi Septemba, mwaka huu, umeme uwe umefikishwa katika Mgodi wa Dhahabu wa Stamigold uliopo Biharamulo.
Alitoa maelekezo hayo jana, Julai 6, 2020 alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kupeleka katika Mgodi huo unaomilikiwa na Serikali.
Akizungumza na viongozi wa Mgodi huo, Dkt Kalemani alimshukuru Rais John Magufuli kwa kutenga fedha za kutosha kuweza kutekeleza Mradi huo mkubwa.
“Nataka nitoe taarifa kwenu watu wa Stamigold, kwamba Mheshimiwa Rais ameshatuagiza kutekeleza Mradi huu. Tunazo shilingi bilioni 9.5 kwa ajili ya kuleta umeme hapa.”
Akieleza zaidi, alisema ujenzi wa Mradi huo utakaotumia takribani miezi miwili na nusu, unatekelezwa kwa fedha za ndani kwa asilimia 100.
Aidha, alieleza kuwa umeme utakaopelekwa Mgodini hapo unatolewa eneo la Mpomvu, mkoani Geita, umbali wa takribani kilomita 100 na kwamba ili kuhakikisha umeme huo unakuwa wa uhakika, zitawekwa transfoma mbili katika eneo husika.
Alisema, Serikali imedhamiria uchimbaji wa madini wa aina zote utumie umeme ili uwe na tija hivyo kuwawezesha wachimbaji kulipa tozo stahiki na kutoa gawio kwa Serikali.
Waziri aliutaka uongozi wa Stamigold, baada ya kufikishiwa umeme, kuandaa mapendekezo ya mahitaji yao ya baadaye ya umeme ili Serikali kupitia Wizara ya Nishati ijipange kuwapatia huduma hiyo.
Awali, akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi kwa Waziri, Kaimu Meneja wa Mgodi, Mhandisi Rashid Lulamka, alisema umeme utakapofikishwa Mgodini hapo, utasaidia kuokoa takribani shilingi milioni 700 kwa mwezi ambazo hutumika kununulia mafuta ya kuendeshea mitambo.
“Kwa sasa, tunatumia takribani shilingi bilioni moja kwa mwezi kwa ajili ya kununua mafuta. Tukipata umeme, matarajio yetu ni kushuka kwa kiwango hicho hadi shilingi milioni 300,” alifafanua.
Katika ziara hiyo, Waziri aliambatana na viongozi pamoja na wataalamu mbalimbali kutoka Wizarani, TANESCO na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
More Stories
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi
Lina PG Tour yafufua gofu Moshi
Kampeni ya Sako kwa Bako yawafikia Kanda ya Kati