November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kufanikisha kiwanda cha kuzalisha vilainishi na mafuta kupata leseni

Na Hadija Bagasha Tanga,

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima amesema serikali ya mkoa kwa kushirikiana na Serikali Kuu, Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kuwa watafanya kila linalowezekana ili mwekezaji wa Kiwanda cha kuzalisha vilainishi na mafuta kwa ajili ya mashine na magari cha Mogas, kilichopo jijini Tanga apate leseni.

RC Malima ameyasema hayo wakati alipotembelea kiwanda hicho mara baada ya kupata malalamiko ya kukwamishwa kwa mwekezaji huyo katika upatikanaji wa leseni.

“Nataka nimhakikishie mwekezaji Mogas serikali itafanya kila linalowezekana ili apate leseni na kila anachohitaji kifanyike ili uwekezaji uende mara mbili. Sasa hao wanaokuja wanatoa taswira kwa watu wengine kwamba Tanga ipo kwa ajili yakupokea mitaji na uwekezaji na wanapeleka ujumbe mzuri kwa watu wengine na serikali ya mkoa tunawaunga mkono kwa asilimia 100.

“Katika Mkoa wa Tanga nimeweka utaratibu wa kuhamasisha wawekezaji kushiriki na sisi moja kwa moja kwenye maendeleo ya serikali ya mkoa, kwa hiyo kama kuna mwekezaji amekuja ana jambo lake urasimu umekuwa mwingi tunataka kuviondoa hivyo.

“Leo kuna mwekezaji amekuja kufuatilia upatikanaji wa vibali akaambiwa asubiri miezi sita na sasa umepita mwezi mmoja na nusu, leo kaja kuniambia Mheshimiwa hatutaki kuwachongea lakini miezi sita kweli, na hicho kibali chenyewe mimi nauliza ni cha kusaini kwa mkono sasa kusaini kwa mkono miezi sita.

“Kwa hiyo sasa hawa wenye matendo ambayo mimi nawaita ya kipuuzi kumzuia mwekezaji ambaye amekuja nchini kwako kwa lengo la kuleta mitaji na mambo mengine, uwekezaji ule ndiyo unaleta ajira za ziada na kodi hata mzunguko wa fedha,” amesema RC Malima.

Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Mogas, Geofrey Rugazoora alisema wanaishukuru serikali mkoani Tanga ambapo pia ameahidi kutoa mchango chanya katika kuchangia maendeleo mkoani hapa.

“Kipekee kabisa tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan ambaye alizindua kiwanda chetu hiki akiwa Makamu wa Rais, lakini pia Serikali ya Mkoa wa Tanga kupitia kwa Mkuu wa Mkoa kwa kusikia kilio chetu. Tunaahidi kutoa ushirikiano na ajira kwa kadri zitakavyopatikana,” amesema.