Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Zanzibar
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Riziki Pembe Juma, amesema Serikali itaendelea kuwawezesha vijana kupata elimu na ujuzi utakaowasaidia kujiajiri na pia kuajirika, ili kujikwamua kiuchumi na kuchangia maendeleo ya taifa.
Akizungumza wakati akifunga mafunzo ya upambaji wa uso (make-up) yaliyofanyika katika ukumbi wa Baytul Yamiin, Bwawani, mjini Unguja, Mhe. Riziki alisema hatua hiyo inalenga kuwawezesha vijana kujiendeleza kimaisha sambamba na kudumisha utamaduni wa Zanzibar.
Alifafanua kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya Awamu ya Nane imekuwa ikichukua hatua madhubuti katika kuinua ajira kwa vijana hususan kwenye sekta zisizo rasmi, kutokana na changamoto za upungufu wa nafasi za kazi katika sekta rasmi.
“Serikali kupitia Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwa kushirikiana na mradi wa SEBEP, imekuwa ikiandaa mafunzo ya aina hii ili kuwajengea vijana, hususan wa kike, uwezo wa kujitegemea na kuondokana na utegemezi,” alisema Waziri Riziki.
Aidha, aliwataka vijana walioshiriki mafunzo hayo kutumia ujuzi walioupata si tu kwa kujipatia kipato, bali pia kwa kuwafundisha wenzao, kuwa mfano wa uadilifu katika biashara na kuwaheshimu wateja wao.
“Mtaaji mkubwa wa taifa letu ni wananchi wake. Mkono wenye ujuzi si wa kuomba, bali ni wa kujikimu na kuchangia maendeleo ya familia na taifa,” alisisitiza Waziri.
Sambamba na hilo, aliwaasa vijana kuendelea kudumisha amani na utulivu kuelekea uchaguzi, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi, ili kila mmoja aendelee na shughuli zake za kimaisha bila bughudha.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (ZEEA), Bw. Juma Burhani Mohammed, alisema taasisi yake itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuwatafutia ajira vijana walionufaika na mafunzo hayo, na kuhakikisha wanaendeleza ujuzi waliopata.
Naye Meneja wa Mradi wa Kujengea Vijana Uwezo wa Kujiajiri na Kuajirika katika Uchumi wa Buluu (SEBEP), Bw. Salum Mkubwa Abdullah, alisema lengo la mradi huo ni kuwapatia vijana stadi zitakazowawezesha kuinuka kiuchumi.
Washiriki wa mafunzo hayo kwa upande wao walieleza dhamira ya kuyatumia mafunzo waliyopewa kwa kujiajiri na kuchangamkia fursa za ajira zilizopo nchini. Pia walimshukuru na kumpongeza mkufunzi wao, Ndg. Emy Broun, kwa kuwafundisha taaluma itakayowasaidia katika maisha yao.
Jumla ya vijana 52 wa kike walishiriki katika mafunzo hayo ya upambaji wa uso, ambapo kati yao vijana 10 wamepatiwa ajira moja kwa moja na mkufunzi wao.

More Stories
Kihongosi amtaka mkandarasi kuwalipa vibarua stahiki zao
DC Mbozi afuturisha wananchi, asisitiza mshikamano na Umoja.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali: Nina imani mubna utendaji kazi wa ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria