January 21, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kuendelea kushirikiana na wadau sekta ya michezo

Na Bakari Lulela, TimesMajira Online

WIZARA ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imesema itashirikiana kwa karibu na wadau wa wadhamini wa michezo watakaojitokeza kuwekeza nguvu zao katika eneo hilo ili kuinua zaidi sekta ya michezo nchini.

Ahadi hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbasi katika hafla Maalumu ya futari iliyoandaliwa na kampuni ya Peak Time Sports Agents ikiwa na lengo la kuwakutanisha kwa kuwapa hamasa mabondia na wadau wa michezo huo pamoja na kumuenzi aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Ngumi za Kulipwa nchini Tanzania (TPBO) Yassin Abdallah Ustadh aliyefariki septemba 7, 2020.

Dkt. Abbass amesema kuwa, mchezo wa masumbwi ni kiwakilishi tosha katika medali za michezo hapa nchini hivyo wadhamini wanatakiwa kujitokeza na kuwekeza nguvu zao katika mchezo huo ambao umekua ukikua na kupendwa na watu wa rika zote.

Jambo kubwa kwa sasa linalotakiwa kufanywa na mabondia hao ni kujiamini katika mapambano yao mbalimbali ya ndani nan je ya nchi ili kuweza kushinda na kuendelea kulitangaza Taifa duniani.

“Wanamichezo wanapaswa kutambua kuwa wao ni wawakilishi muhimu wa Taifa na kwamba Serikali kwa sasa ipo karibu na wanamichezo na tayari imeshaanza kutenga fedha kusaidia wanamichezo wanaoshiriki michezo mbalimbali ya kimataifa,”.

“Serikali kwa sasa haitoi tu bendera kwa wanamichezo, tunatoa pia fedha na vitu vingine kwa ajili ya wanamichezo huku ikifanya mageuzi makubwa kwani imeshaondoka kuwa msimamizi tu wa Sera za Sekta za Michezo na kuwa pia mapromota kabisa wa michezo kama hii ya ngumi Tanzania ili kuweza kupata mabondia watakaotuwakilisha vyema kwenye michezo ya kimataifa,” amesema Dkt. Abbasi.

Kwa upande wake sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadj Mussa Salum aliwapongeza wadau hao na kusema kuwa, ni faraja na baraka ya kuwakutanisha katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa kufuturu na wanatasnia hao.

“Kufunga si kujizuia na kula tu bali ni kujizuia na mambo mbalimbali hii ndio baraka ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani watu kusaidiana, kukirimiana pamoja na kukisoma kitabu cha Quran kwa wakati wote wa mwezi huu,” amesema kiongozi huyo.

Mwakilishi wa mchezo wa ngumi za kulipwa Tanzania, Yahya Pori amewataka waandaaji wa hafla hiyo kutoishia tu kwenye mwezi huu wa Ramadhani bali liwe endelevu katika kuendeleza tasnia ya ubondia hapa nchini.

Muandaaji wa hafla hiyo, Kapteni Selemani Semunyu amewashukuru wadau wote wa mchezo huo sambamba na wadhamini kwa kujitokeza kwa wingi kuendeleza tasnia ya masumbwi na kusema hiyo ni moja ya njia ya kuinua vipaji vya vijana hapa Tanzania.