March 10, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kuendelea kupeleka huduma kwa Wananchi

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online-Mwanza

SERIKALI itaendelea kupeleka huduma bora kwa wananchi na kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini, ili kuboreshewa maisha yao.

Hayo yamesemwa leo Machi 10, 2026 na Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenan Kihongosi wakati akikagua mradi wa ujenzi wa daraja la Sukuma lililopo Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, akiendelea na ziara yake yenye lengo la kukagua uhai wa chama, utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo,kusikiliza na kutatua kero za wananchi kupitia mikutano ya hadhara.

Mradi huo ambao unajengwa kwa kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 9,fedha zilizotolewa na Serikali,umefikia asilimia 80 ya maendeleo ya ujenzi na unatarajia kukamilika ifikapo Aprili 16, mwaka 2026.

Akizungumza mara baada ya kufika katika eneo hilo la mradi kwa lengo la kukagua mradi huo Kihongosi,amesema, ameridhishwa kwa asilimia 100 na ubora wa kazi iliyofanyika na kuwataka wananchi kulinda miundombinu hiyo ili iweze kudumu.

Kihongosi amewahimiza wananchi wa Mwanza kuendelea kushirikiana na chama hicho na Serikali katika kulinda na kuendeleza miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao.