November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kuendelea kupambana na ujangili

Na Martha Fatael, TimesMajira Online, Moshi

MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu amesema serikali haitasita kutaifisha Mifugo na mali nyingine zitakazokamatwa katika hifadhi ya Taifa ya mlima Kilimanjaro (KINAPA) kinyume cha sheria.

Aidha serikali imewaonya watu wanaofanya Vitendo vya ujangili katika hifadhi hiyo na kwamba wale wote wenye Nia ya kuua wanyamapori na kuvuna maliasili nyingine wajihadhari.

Mkuu wa mkoa amesema hayo wakati akipokea timu ya watu zaidi ya 200 waliopanda mlima huo katika maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru.

Amesema serikali haiwezi kuvumilia matukio ya moto katika mlima huo pamoja na Ukataji miti na kwamba serikali itachukua hatua za kisheria.

Amesema kati ya watu 200 wakiwamo mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika baadhi ya nchi, ni wapanda mlima 101 pekee ndiyo waliofanikiwa kufika vilele vya juu vya mlima ikiwamo Uhuru peak.

Babu amesema kitendo cha baadhi ya mabalozi wakiongozwa na Dkt Asha Rose Migiro kupanda mlima huo ni sehemu ya kutangaza fursa za utalii hapa Nchini.Mapema balozi Asha Rose amesema kupanda mlima ni sehemu ya kutangaza utalii katika nchi wanazowakilisha.

Kwa upande wake kiongozi wa waliopanda mlima Meja Jenerali Salum Numbe ameomba serikali kwa kushirikiana na makampuni ya utalii kuona namna ya kuwasaidia wapagazi ( wagumu ) kupata bima za afya.Amesema lengo ni kuwapatia uhakika wa afya zao wanapokuwa wakitekeleza shughuli za mlima.