May 4, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kudhibiti utoroshaji wa Madini,mapato

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

SERIKALI  kupitia Wizara ya Madini imefanikiwa kudhibiti kwa kiasi kikubwa vitendo vya utoroshaji wa madini nchini, hali iliyosaidia kuongeza mapato ya Serikali na kulinda rasilimali za taifa. Hatua hizi ni sehemu ya mkakati mpana wa kuimarisha mchango wa sekta ya madini katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

Aidha ,Serikali inakwenda kufanya mabadiliko makubwa sana kwenye mgodi wa Mirerani katika kudhibiti upotevu wa Madini na upotevu wa mapato

Waziri wa Madini Anthony Mavumde ameyasema hayo Bungeni jijini Dodoma  wakati akiwasilisha bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka 2025/2026 ambapo alisema, wathaminishaji  wanaokwenda  chini ya mgodi kufanya uthaminishaji wa mapato kuanzia Julai Mosi watapewa kofia ngumu zenye kamera  na zenye microphone.

“Kwa hatua hii ,mthaminishaji akiwa kule chini   mgodini Mimi nikiwa wizarani ofisini nitakuwa namuona anachokisema na ambacho tunakiona ,lengo ni kudhibiti mapato na kupunguza utoroshaji wa Madini ya Tanzanite.” Amesema Mavunde

Aidha Mavunde amesema  kuwa kati ya Julai 2024 na Machi 2025, Serikali imefanikiwa kukamata madini ya thamani ya shilingi bilioni 17.76 yaliyokuwa yakitoroshwa katika mikoa mbalimbali ikiwemo Geita, Ruvuma, Kahama, Mwanza, Shinyanga, Kagera, Dar es Salaam, Mirerani, Simiyu, Singida, Chunya, Arusha na Lindi. Watuhumiwa 75 wamefikishwa kwenye vyombo vya sheria, na madini hayo yamechukuliwa na Serikali.

“Ni rai yangu kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kujiepusha na vitendo vya utoroshaji kwani vina madhara makubwa kwa biashara zao na kwa Taifa kwa ujumla,” alisisitiza Waziri Mavunde.

Mapato yaongezeka kwa asilimia 43

Kwa upande wa mapato amesema , Wizara imekusanya jumla ya shilingi bilioni 783.88 hadi Machi 2025, ikilinganishwa na bilioni 548.30 zilizokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka uliopita. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 42.97 – mafanikio yanayoonesha ufanisi wa mikakati ya Serikali katika usimamizi wa rasilimali za madini.

Amesema katika kuhakikisha sekta ya madini inazidi kuwa na mchango mkubwa kwa uchumi wa Taifa, Tume ya Madini imetoa leseni mbalimbali za shughuli za uchimbaji na uchenjuaji madini, zikiwemo leseni Moja ya uchimbaji mkubwa ,leseni tatu za uchimbaji wa kati,leseni 275 za uchimbaji mdogo,leseni 58 za utafiti na leseni tatu za uchenjuaji.

Amesema Madini yanayolengwa ni pamoja na graphite, nickel, cobalt, lithium, heavy mineral sand na rare earth elements.

Waziri Mavunde amesema  kuwa Serikali haitatoa leseni za uchimbaji wa kati au mkubwa kwa madini muhimu na ya mkakati kwa mwekezaji yeyote asiyekuwa na mpango madhubuti wa kuongeza thamani ya madini hayo ndani ya nchi. Tayari kampuni ya Duma Tanzgraphite Limited (DTL) imepata leseni ya uchimbaji wa madini ya kinywe (graphite) katika eneo la Epanko, Wilaya ya Ulanga.

“Tunahitaji kuona Tanzania inanufaika ipasavyo na madini iliyo nayo. Hii inamaanisha si tu kuyatoa ardhini, bali pia kuyachakata na kuongeza thamani kabla ya kuuza nje ya nchi,” alimesisitiza Waziri.

Vipaumbele vya Wizara kwa 2025/2026

Kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Wizara ya Madini imepanga kutekeleza vipaumbele vya Wizara hiyo vitakavyotekelezwa katika kipindi hicho  kwa lengo la kuongeza ukusanyaji wa maduhuli hadi kufikia shilingi trilioni 1.41.

Amevitaja vipaumbele hivyo kuwa ni pamoja na  kuhamasisha uwekezaji na uongezaji thamani wa madini,kuimarisha usimamizi wa minada na maonesho ya madini ya vito na kurasimisha na kuwaendeleza wachimbaji wadogo, hasa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.

Wizara ya Madini imeomba na kupitishiwa na Bunge  bajeti ya shilingi bilioni 224.98 kwa ajili ya matumizi ya Wizara hiyo  na taasisi zake kwa mwaka wa fedha 2025/2026.