November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kuboresha elimu nchini

Na Hadija Bagasha, Timesmajira Online,Tanga

SERIKALI imetangaza mkakati wa uboreshaji wa elimu nchini ambapo walimu ambao wataajiriwa ni wale wataokuwa wamefanya mitihani yao na kufaulu vizuri tofauti na ilivyokuwa awali wizara ilikuwa ikijaza nafasi zilizokuwa zikihitajika bila kupitia mchakato huo .

Profesa Mkenda ameyasema hayo Mei 30,2024 jijini Tanga wakati wa uwasilishaji wa taarifa ya hali ya ufaulu na ujifunzaji wa wanafunzi ulioshirikisha wadau mbalimbali wa elimu wakiwemo Maofisa Elimu mikoa, Halmashauri,Wakurugenzi na Taasisi.

Amesema kwamba wanaona jambo hilo sio jema kwao lakini wajiulize kwanini madaktari wanapomaliza Shahada ya kwanza wanalazimika kufanya mitihani ndio wanafanya kazi hivyo suala hilo linapelekwa kwa walimu ili kuweza kupata walimu bora.

Profesa Mkenda amesema kwamba wanaamini kigezo hicho ndio ambacho kitalivusha taifa na watahakikisha wanachukua walimu waliobora zaidi na watakaofanya mitihani na kufaulu vizuri.

“Kama tunataka tuboresha elimu lazima twende kwa ujasiri tunapojaribu kuajiri Walimu tujiulize tunapigania mwanao apata Mwalimu bora sasa tutakapo ajiriwa lazima wafanye mtihani na watakaofeli hawatapata nafasi,”amesema.

Pia amesema Walimu waliopo watalindwa mpaka watakapostaafu na wataendelea kuwajengea uwezo kwani Rais anatenga fedha nyingi kwenye elimu.

“Tathimini tunayoifanya lazima iendelee na hatua nzuri za baraza hatufurahii kufutia mitihani watahaniwa na waliojaribu kuiba mitihani,”amesema .

Aidha amesema kwa sasa wapo kwenye mchakato wa sheria mpya ambayo itawabana watu watakaobainika kuiba mitihani watakamatwa na kushtakiwa kwa kesi za uhujumu uchumi.

“Katika jambo hilo tuzidi kuwa makini Necta msilegeze kamba nendeni mkahakikishe mnalisimamia na takwimu ni muhimu zitatueleza vizuri tunakwendaje na katika hilo tunataka kuimarisha takwimu za elimu Tanzania na kazi hii imeanza na timu ipo kazini,”amesema Profesa Mkenda

Awali Katibu Mkuu Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof. Caroline Nombo amesema taarifa ya tathimini ya ujifunzaji kwa wanafunzi wa kidato cha pili iliowasilishwa na Baraza la Taifa Mitihani (Necta) inatoa picha halisi kuhusu ufundishaji na ujifunzaji kwa shule za sekondari na msingi nchini.

Hivyo mapendekezo yaliyotolewa yanaonesha dira ya nini cha kufanya ili kuhakikisha ufundishaji,ujifunzaji na tathimini katika ngazi ya shule unaimarika.

Amesema Wizara hiyo itaendelea kushirikiana bega kwa bega na wadau wote wa elimu na baraza la mitihani kuhakikisha masuala yote ya ufundishaji na tahimini yanaimarishwa kwa lengo la kukuza umahiri wa wanafunzi katika masomo hayo.

“Wizara kupitia Baraza la Mitihani tutaendelea kuhakikisha kuwa tathimini ya ujifunzaji wa wanafunzi wa kidato cha pili awamu ya pili ya mwaka 2025 itafanyika kwa ufanisi mkubwa,”amesema

Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani nchini (NECTA) Dkt Said Mohamed amesema suala la kufanya tathimini ni muhimu ili kuboresha kiwango cha elimu na wamekuwa wakifanya katika maeneo mbalimbali lengo ni kutaka kujua maendeleo ya wanafunzi wamesoma na wanataka kufika wapi.

Amesema wameanza kufanya tathimini kwa masomo manne ambapo wameanza Hisabati,Sayansi huku akieleza kwamba katika somo hilo katika mtihani wa darasa la saba mwaka huu utakuwa hauna maswali ya kuchagua.

Aidha amesema hali ya ufaulu nchini ukiangalia takwimu za upimaji wa darasa la nne kwa miaka 10 ufaulu wa jumla umekuwa juu ya asilimia 80 itapanda kidogo na kushuka.

“Mfano mwaka 2015 darasa la nne Watahiniwa walikuwa laki tisa sasa kwenye usajili wanafikia mpaka 1,800,000 na ufaulu umeendelea kubakia asilimia 80 namba ya watahiniwa imeongezeka mwaka hadi mwaka,”.

Katibu huyo amesema kwa upande wa darasa la saba ufaulu ulikuwa ni asilimia 67 mwaka 2015 na umeendelea kupanda na kufikia asilimia 80 mwaka 2023 kimahesabu huo ni ufaulu unaoafanana na bado wameendelea kufika asilimia 80.

Huku akieleza kuwa kwa upande wa sekondari kidato cha pili ufaulu 2015 mpaka 2023 umekuwa ukiongezeka kutoka asilimia 67 2015 mpaka kufikia asilimia 89 mwaka jana.