Na Bakari Lulela,Timesmajira,Online
SERIKALI imesema jicho lake liko kwenye Bandari ya Dar es Salaam kwa kuwa ni eneo muhimu katika maendeleo ya uchumi wa nchi na ni lango kuu la kibiashara.
Amesema sehemu kubwa ya mapato ya nchi yanapatikana kupitia bandari hiyo, hivyo Serikali ya Tanzania haitaki masihara na yeyote atakaethubutu kuleta mzaha.
Kauli hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara alipofanya ziara kwenye Ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na kuzungumza na Menejimenti ya Mamlaka hiyo.
Katika ziara hiyo ambayo amehimiza huduma nzuri kwa wateja na kukemea uwepo wa makundi miongoni mwa wafanyakazi katika bandari hiyo, ambayo amesema yanaweza kuathiri ufanisi wa utoaji huduma.
“Wateja wanapohudumiwa vizuri wanakuwa mabalozi wa kupeleka ujumbe mzuri kwenye nchi jirani kwa kuwaambia wengine kuwa huduma katika Bandari ya Dar es Salaam ipo vizuri,” amesema Waitara.
Waitara amewataka wafanyakazi wote wa TPA, kuanzia uongozi wa juu mpaka langoni, kutambua kwamba serikali pamoja na wananchi wanawategemea katika utendaji wa majukumu yao.
Hata havyo amesema wanapotoa huduma, wajue wanatoa huduma kwa niaba ya Watanzania wengi wanaotazama kazi yao waone ni nzuri.
“Rais Samia Suluhu Hassan, anaposema tunataka fedha safi na kodi ambayo si ya kushurutisha na kufilisi watu, anamaanisha watu ambao mmesimama mahali ambapo kuna biashara, ifanyike biashara halali,” amesema.
Naibu Waziri huyo, pia amekemea uwepo wa makundi miongoni mwa wafanyakazi na kudai anataarifa za kundi linalojiita wenyeji wenye bandari yao na kundi linaloitwa wakuja, ambapo alisema wanaotumia kauli hiyo, serikali haitaki kuzisikia.
Katika hatua nyingine, Waitara ameitaka TPA kushughulikia matatizo ya tozo za nauli katika kivuko cha Buchosa kilichopo mkoani Mwanza na Nyamisati kilichopo Mafia ambako wananchi wanalipa sh. 1,200 kitu ambacho Rais Samia alishaagiza kifanyiwe kazi.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu