May 28, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali inavyosimamia machinga

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

KATIKA  jitihada za kuendeleza uchumi wa wananchi wa kipato cha chini, Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imeendelea kusimamia kikamilifu shughuli za wafanyabiashara ndogondogo kama vile machinga, mama/baba lishe, waendesha bodaboda na bajaji, washonaji nguo na wasusi.

Akizungumza leo Mei 27,2025 Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha bajeti ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,wananwake na Makundi Maalum Dkt.Dorothy Gwajima amesema,hili limefanyika kwa kuzingatia umuhimu wao katika ustawi wa jamii na ajira nchini.

Amesema , hadi kufikia tarehe 8 Mei 2025, jumla ya wafanyabiashara 78,984 walikuwa wamesajiliwa rasmi kupitia mfumo wa kidigitali.

Waziri huyo amesema,kati ya hao, wanawake walikuwa wengi zaidi wakiwakilisha asilimia 63  ya wananwake ambao ni  50,283 huku wanaume wakiwa asilimia 37 ambao idadi yao ni  28,701.

“ Hatua hii ya usajili imerahisisha utoaji wa vitambulisho vya kidigitali vinavyowawezesha kupata huduma za mikopo yenye masharti nafuu kutoka Benki ya NMB.”amesema Dkt.Gwajima

Vile vile amesema, Serikali imeonyesha dhamira ya dhati katika kuwawezesha wafanyabiashara hawa kwa kuboresha miundombinu.

Amesema,tangu mwaka 2022, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, alitoa kiasi cha Shilingi Milioni 10 kwa kila mkoa kwa ajili ya ujenzi wa ofisi maalum za wafanyabiashara ndogondogo.

“Hadi kufikia Aprili 2025, mikoa 17 kati ya 26 ilikuwa tayari imekamilisha ujenzi wa ofisi hizo ambazo ni nyenzo muhimu katika kusaidia kuratibu shughuli za kiuchumi, kutoa mafunzo, na kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara wadogo.”amesisitiza

Kwa mujibu wa Waziri Gwajima,mpango huu unaonyesha msukumo mpya wa Serikali katika kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma kwenye safari ya maendeleo.

Amesema,kwa kuweka mifumo ya kidigitali, kuongeza upatikanaji wa mikopo, na kuboresha miundombinu, Serikali inaweka mazingira bora kwa wafanyabiashara wadogo kukua, kushindana na hatimaye kuchangia kwa kiwango kikubwa katika pato la taifa.