November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali inavyoenzi falsafa za watangulizi wake kwa kuimrisha ushirikiano na SADC

Na Penina Malundo,TimesMajira,Online

SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, kama ulivyo utamaduni wa nchi ya Tanzania imeendelea kushirkiana na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) katika kuhakikisha inatumia fursa mbalimbali ambazo nchi za SADC inazitoa ikiwemo suala la ukuaji wa uchumi na uimarishaji wa Amani na Upendo baina ya nchi moja na nyingine.

Pia imeendelea kuzienzi falsafa zilizoachwa na watangulizi wake wa awamu zilizopita katika Serikali ya Tanzania,ikiwemo ya Rais wa Kwanza Mwalimu Julius Kambarage Nyerere hadi Rais wa sasa Samia Suluhu Hassan kuhakikisha inaendeleza ushirikiano wake na nchi nyingine 15 za SADC katika sekta mbalimbali.

Miongoni mwa maeneo ambayo yameendelea kutilia mkazo ni katika maeneo ya uimarishwaji ulinzi na usalama katika nchi wanachama pamoja na fursa mbalimbali za kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Jumla ya nchi wananchama wa SADC ni 16 ikiwemo Tanzania, Angola, Botswana, Comoro, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Eswatini, Lesotho, Madagascar, Malawi, Mauritius, nyingine ni Msumbiji, Namibia, Ushelisheli, Afrika Kusini, Zambia na Zimbabwe.

Hivi karibuni Rais Samia,aliungana na wakuu wa nchi na Serikali ya SADC, katika mkutano wa dharura uliofanyika Mji wa Maputo nchini Msumbiji, ambapo umefanyika sambambana na maadhimisho ya miaka 40 tangu kuanzishwa kwa jumuiya hiyo, ikiwa na kaulimbiu; ‘Kuimarisha Amani na Usalama, Kuhamasisha Maendeleo na Ustahamilivu wa Changamoto Zinazoikabili Dunia.’

Rais Samia amepata wasaa wa kukutana na viongozi na wakuu wengine wa nchi wanachama 15 na kujadili ajenda mbalimbali zikiwemo zinazohusu mtangamano wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo, fursa mbalimbali za kiuchumi pamoja na changamoto za kiusalama.

Katika mkutano ulioongozwa na Mwenyekiti wa SADC Rais wa Msumbiji,Filipe Nyusi anasema jitihada za pamoja kutoka nchi wanachama wa ukanda wa SADC zinahitajika zaidi katika kukabiliana na tatizo la ugaidi linaloikabili nchi hiyo, kwani limekuwa likirudisha nyuma juhudi za maendeleo kwa Msumbiji na nchi wanachama.

Anabainisha kuwa,mkutano huo ulikuwa wa dharura ambapo umezungumzia mambo mbalimbali ikiwemo maambukizi ya ugonjwa unaosababishwa na virusi vya Corona (UVIKO 19), uanzishwaji wa kituo cha majanga, masuala ya mabadiliko ya tabianchi, usalama wa chakula, biashara na uwekezaji katika ukanda wa SADC.

Rais Nyusi anazizisisitiza nchi wanachama kuendelea kuunga mkono jitihada za taasisi za utafiti katika kufuatilia taarifa za kusambaa kwa UVIKO 19 na mawimbi mapya ya ugonjwa huo na kuendelea kuchukua tahadhari ili kuzuia maambukizi mapya.

Akizungumzia changamoto za mabadiliko ya tabianchi, Rais Nyusi anasema baadhi ya nchi wanachama zimekumbwa na uhaba wa mvua na nyingine kupata mvua nyingi zaidi na kufanya uwepo wa uwezekano kwa baadhi ya nchi kukumbwa na uhaba wa chakula.

Katika hatua nyingine, itakumbukwa kuwa mnamo Aprili 23, 2021 Rais Samia Suluhu Hassan alikutana na Katibu Mtendaji wa SADC, Dk. Stergomena Tax ambapo alipata fursa ya kupokea taarifa juu ya masuala mbalimbali yahusuyo jumuiya hiyo.

Mazungumzo hayo yalifanyika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula.

Akitoa taarifa yake, Dkt.Tax ambaye anamaliza muda wake wa miaka minane ifikapo Agosti 2021,aliishukuru Tanzania kwa ushirikiano alioupata wakati akiwa Katibu Mtendaji wa SADC.

Dkt.Tax anasema Tanzania ambayo wakati wa uenyekiti wake wa SADC iliandaa na kukamilisha mkakati wa maendeleo wa SADC licha kuwepo kwa changamoto la janga la Korona duniani.

Anasema katika uongozi wake wa uwenyekiti wa SADC,Tanzania imefanikiwa kukifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya SADC, kuanza mradi wa uwekaji sanamu ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika Umoja wa Afrika (AU) na uendelezaji wa gesi asilia.

Aidha, anasema katika kipindi hicho SADC imeendelea kuwa na utulivu wa kisiasa ambao umetoa fursa nyingi za maendeleo ya kiuchumi.

“Natoa wito kwa Tanzania kutilia mkazo katika uimarishaji wa sekta za uzalishaji kama vile viwanda, kilimo, biashara, kusimamia ubora na kuendeleza miundombinu ili kuweza kutumia fursa za maendeleo ya kiuchumi kwa nchi za SADC,” anasema Dk. Tax.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akielezea ushirikiano wa Tanzania na nchi za SADC anasema Tanzania tangu mapigano yanayoendelea Kaskazini mwa Msumbiji na Kusini mwa Tanzania katika jimbo la Cabo Delgado yameanza nchi za SADC na viongozi wa nchi hizo wamekuwa wakikutana katika kutafuta suluhu ya kuleta amani na usalama endelevu katika eneo hilo.

“Tumekuwa mstari mmoja tukisaidiana na nchi za SADC kuangalia ni jinsi gani ya kupambana na vitendo vya ugaidi kama vinavyotokea huko Msjmbiji,” anasema Balozi Mulamula na kuongeza:

“Nchi yetu inashirikiana na nchi za SADC katika kuimarisha mambo mbalimbali ikiwemo suala la ulinzi na usalama na kuhakikisha tunachukua hatua madhubuti za kuimarisha ulinzi wa mipaka yetu.”anasema Balozi Mulamula

Huu ni mwanzo mzuri kwa Serikali ya Awamu ya Sita ndani ya SADC, ambapo kitu pekee ambacho wananchi watamzawadia Rais Samia Suluhu Hassan ni kuchapa kazi kwa bidii na kuchangamkia fursa za SADC yenye zaidi ya raia milioni 345 katika eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba9,882,959.