Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Zanzibar
RAIS wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt.Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa serikali inahitaji mchango wa wadau mbalimbali kuweza kukabiliana vizuri na mapambano dhidi ya vitendo vya udhalilishaji katika jamii, ambavyo vimeonekana kushamiri katika siku za hivi karibuni.
Rais Mwinyi ameyasema hayo leo wakati wa tukio la uzinduzi wa mfumo wa kanzi data (Database system) kwa ajili ya kukusanya takwimu sahihi za mapambano dhidi ya vitendo vya udhalilishaji kwa wanawake na watoto katika kongamano la harakati za kutokomeza vitendo vya udhalilishaji Zanzibar.
Rais Mwinyi ameeleza kuwa serikali ndio yenye jukumu la kusaidia kujenga ustawi wa wananchi wake, lakini jambo hilo limekuwa ni changamoto, hali inayohitaji nguvu ya pamoja kutoka kwa wadau wengine ambao wanaweza kusaidia kuboresha sekta ya maendeleo ya jamii, na hasa katika kukabiliana na vitendo vya udhalilishaji.
“Suala hili la udhalilishaji wa wanawake na watoto linawagusa wadau wengi. Zipo taasisi za serikali zinahusika nalo lakini pia zipo taasisi binafsi. Tunahitaji nguvu ya pamoja sote kukabiliana na hili.” amesema Rais Mwinyi.
Akizungumza pia katika kongamano hilo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Legal Services Facility-LSF) nchini Tanzania, Lulu Ng’wanakilala ameiomba Serikali Mapinduzi Zanzibar, iweke mikakati ya kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia kupitia mijadala na makongamano mbalimbali yanayoandaliwa kwa kushirikisha wadau muhimu wa maendeleo ya jamii visiwani humo.
Ng’wanakilala ameiomba Serikali pamoja na wadau wa kutetea haki za binadamu, watumie fursa ya kongamano hilo, kupata muarobaini wa vitendo hivyo, vinavyoongoza kuathiri kuwanawake.
“Kongamano hili liwe fursa kwa wadau, katika kuweka mikakati thabiti dhidi ya ukatili wa kijinsia,” amesema Ng’wanakilala.
Mtendaji huyo wa LSF amesema, kumekuwa na vitendo vya ukatili wa kijinsia, ambapo kwa wanawake na watoto.
“Ripoti yetu inaonyesha katika kila matukio (4) ya ukatili yaliyoripotiwa na wanawake yalihusisha unyanyasaji wa kijinsia, ambapo visa vyote vilivyoripotiwa vinakadiriwa kufikia asilimia 26.5 kwa mwaka 2020,”
“Hii inaonesha changamoto kubwa ya upatikanaji haki, hasa kwa wanawake wanaokutana na ukatili kwenye shughuli za uchumi na nyumbani,” amesema Ng’wanakilala.
Ng’wanakilala amesema, LSF itaendelea kushirikiana na Serikali na wadau wengine wa utetezi wa haki za binadamu, kutetea haki za wanawake na makundi maalumu, yanayoongoza kwa kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
“LSF kama mdau katika sekta ya upatikanaji haki na msaada wa kisheria, tutaendelea na ushirikiano na kuwa tuna amini katika nguvu ya pamoja kwenye kujenga mazingira rafiki kwa wanawake wote na kutetea kundi la watoto,” ameongeza Ng’wanakilala.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Jumuiya ya Wanawake Wanasheria Zanzibar (ZAFELA), Jamila Mahmoud Juma, amesema kuwa hali ya vitendo vya udhalilishaji katika jamii kwa sasa bado ipo kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na zamani licha ya jitihada mbalimbali kufanyika.
“Tumegundua kuwa ili kuwasaidia wanawake wasidhalilike ni lazima wawezeshwe kiuchumi. Hivyo sisi kama ZAFELA tunatoa mafunzo ya uwezeshaji kiuchumi kwa wanawake ili waweze kujitegemea. Vilevile, tunatoa elimu na msaada wa kisheria kwa wanawake wanakumbana na vitendo vya udhalilishaji,” amesema Mkurugenzi wa ZAFELA.
More Stories
Tanzania kuwa mwenyeji Mkutano wa Kimataifa matumizi bora ya Nishati
Madiwani Ilala watoa chakula kwa watoto yatima
Waziri Mkuu: Tumieni matokeo ya tafiti za kisayansi katika utekelezaji wa mipango ya kitaifa