November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali imetakiwa kumsimamia mkandarasi daraja la JPM

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

KAMATI ya  Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeiagiza serikali kuwasimamia wakandarasi wanaotekeleza mradi wa ujenzi wa daraja la JPM eneo la Kigogo –Busisi Mkoani Mwanza ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati.

Pamoja na kuwasimamia wakandarasi hao watenge fedha kwa ajili ya huduma za jamii katika eneo unapotekelezwa mradi huo ili huduma hizo ziweze kuwanufaisha wananchi.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu wakitazama daraja la JPM lililopo Kigongo-Busisi ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 42 wakati Kamati hiyo ilipofanya ziara ya kutembelea mradi huo pamoja na kivuko cha Mv.Sengerema na Mv.Misungwi.

Hayo yamezungumzwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo Seleman Kakoso wakati kamati hiyo ilipotembelea na kujionea ujenzi wa daraja hilo ambalo kwa sasa limefikia asilimia 42.

Kamati hiyo ya Bunge ya Miundombinu ambayo imefika eneo hili linapojengwa daraja la JPM lenye urefu wa kilomita 3 ambalo litaunganisha barabara ya Usagara –Sengerema hadi Geita katika Ziwa Victoria hadi kukamilika kwakwe litagharimu zaidi ya bilioni 716.

Kasoso amepongeza  jitihada ambazo zimefanywa katika mradi huo ambao  Rais Samia ameendelea kuutekeleza pamoja na Wizara kwa usimamizi mzuri ambao imefanya ya kusimamia TANROADS na TANROADS wamefanya vizuri kuwasimamia wakandarasi.

Amesema mambo ya kuzingatiwa katika mradi huo ni pamoja na kuhakikisha Mkandarasi anatekeleza mradi huo  na anaukamilisha kwa muda ambao wamekubaliana.

 “Jambo hili lisimamieni ili kufanya serikali isiingie gharama ya mara kwa mara kwani Wakandarasi wengi  wanachelewa pale wanapoona kwamba wanahitaji kuongeza mkataba hasa kwenye fedha zile wanazokuwa wanadai,jambo ambalo kwa sasa serikali imeanza kutoka kule,nimeona kila mradi tunaouangalia serikali imeshapeleka fedha,

kwa hiyo tunawaomba msimamie kuliko kwamba mkandarasi anamaliza anaanza kutudai serikali,baada ya mradi  uliopo wa bilioni 690 unaweza kufika hadi bilioni 800,” amesema Kasoso.

Sanjari na hayo Kakoso akaagiza maslahi ya wafanyakazi  waliopo katika ujenzi wa daraja hilo yasimamiwe pamoja na usalama pahala pa kazi ili kulinda usalama kwa wafanyakazi hao.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumuudumu ya Bunge ya Miundombinu Seleman Kasoso, watano kutoka kushoto akiwa na wajumbe wa Kamati hiyo pamoja watendaji wa TANROADS,mara baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa daraja la JPM lililopo Kigongo-Busisi.

Akitoa taarifa ya ujenzi wa daraja hilo kwa kamati hiyo , Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS)Mhandisi Rogatus Mativila amesema pindi daraja hilo litakapokamilika litasaidia suala la usafiri na usafirishaji pamoja na kukuza uchumi wa ukanda huo.

 Mativila amesema mpaka sasa ujenzi umefikia asilimia 41.59  ambapo  mkandarasi ameshatumia siku 753 kati ya siku 1,461 na   ameishalipwa jumla ya bilioni  194 ikiwa ni pamoja na malipo ya awali ya bilioni 87 kwa hati za malipo ambapo mradi huo  ni moja ya miradi ya kimkakati ya serikali ya kurahisisha usafiri na kuleta maendeleo ya kiuchumi na jamii.

Kamati hiyo ya kudumu ya bunge ya miundombinu imekagua kivuko cha MV Sengerema kinachofanya safari zake Kigongo –Busisi pamoja na ujenzi wa daraja la JPM mkoani humo.