January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali awamu ya sita yafanikiwa katika utunzaji mazingira

Na Zena Mohamed, TimesMajira Online Dodoma.

MKUU wa Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo-Dodoma (LGTI),Dkt.Mpamila Madale,amesema pamoja na mafanikio mengine makubwa katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Chuo kimefanikiwa kuboresha na kutunza mazingira kwa kupanda miti zaidi ya 1000  hali inayosaidia kuweka mandhari safi na kuunga Mkono juhudi za Rais katika masuala ya mazingira.

Amesema  katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya awamu ya sita chuo kimepata mafanikio makubwa ikiwemo  kujenga madarasa mapya,nyumba za watumishi, jengo la utawala na Cumpus ya Dodoma ili kuwezesha huduma bora zitakazo wajengea wananchi uwezo wa kuimarisha utawala bora kwa ambapo zaidi ya bilioni 1.8 zimetumika katika ujenzi huo.

Dkt.Madale ameeleza hayo wakati akiongea na Waandishi wa habari chuoni hapo kuhusu mafanikio yaliyopatikana LGTI ndani ya mwaka mmoja wa Rais Samia na kueleza lengo la kufanya hivyo ni kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya sita katika sekta ya elimu huku wakijipanga kutoa wahitimu ambao watakuwa na uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa.

“Tunashkuru  Serikali ya awamu ya sita kwa kutambua umuhimu wa kuwafikia walengwa wa elimu,kwakutupatia eneo lililokuwa Ofisi ya zamani ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ili kujenga kampasi kubwa ya kisasa,LGTI tunamshukuru sana,na niseme wazi kuwa tuna imani naye na tutashirikiana naye bega kwa bega kufanikisha lengo la Serikali katika kutoa huduma bora,”amesema

Kwa upande wake,Naibu Mkuu wa Chuo hicho,Taaluma,Utafiti na Ushauri,Dkt.Michael Msendekwa amesema wameongeza baadhi ya kozi pamoja na kuwapeleka wafanyakazi kwenda kusoma zaidi ili kuongeza ubora wa elimu katika chuo hicho.

Hivyo wamejipanga kuendelea kutoa elimu yenye ubora ikiwa ni pamoja na kuiweka sawa mitaala ambayo itawafanya wanafunzi watoke wakiwa na uwezo wa kujiari na kuajiriwa.

“Chuo kimejipanga kukabiliana na changamoto ya ukatili wa kijinsia ambao umeendelea kujitokeza katika jamii kwa kuongeza baadhi ya kozi ambazo zitasaidia kulinda mmonyoko wa maadili,”amesema

Kuhusiana na mafaniko mengine Naibu Mkuu wa Chuo hicho ,Mipango,Fedha na Utawala,Mashala Yusuph ameyataja mafanikio mengine ni kuongeza idadi ya watumishi kutoka 203 hadi 216 kwa mchanganuo wa wanaume 83 na wanawake 133.

“Ndani ya mwaka mmoja wa Rais Samia watumishi 44 chuo kimewapeleka masomoni kati yao 21 wanasoma shahada ya uzamivu,10 wanasoma shahada ya uzamili na 13 wanasoma shahada ya kwanza na wengine 8 wamemaliza na kuripoti kazini kati ya hao 2 wamehitimu shahada ya uzamivu,4 shahada ya uzamili na 2 shahada ya kwanza,”amefafanua