Na Mary Margwe, Timesmajira Online,Babati
Mkuu wa Mkoa wa Manyara Queen Sendiga, amemuapisha Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Michael Semindu,baada ya kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Januari 25,2025 kuwa Mkuu wa Wilaya hiyo.
Hafla ya uapisho huo imefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mjini Babati huku viongozi mbalimbali wa Serikali,vyama vya siasa na wa dini waliohudhiria hafla hiyo.
Sendiga amesema,anatambua kuwa kila mmoja amejiwekea vipaumbele vyake kama Mkuu wa Wilaya husika, hivyo kama Mkoa pia una vipaumbele vyake ambavyo kila mmoja anatakiwa kuvielewa na hatimaye kuweza kuvitekeleza.
“Wakuu wa Wilaya Mimi kama kiongozi wenu, nina vipaumbele nilivyojiwekea ili kufikia malengo ikiwa ni pamoja na ukusanyaji wa mapato ili Serikali iweze kuwahudumia wananchi na kuleta maendeleo katika Taifa. Kipaumbele cha pili ni kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi kuanzia ngazi ya mtaa mpaka katika Halmashauri zao,”amesema Sendiga na kuongeza:
“Kipaumbele cha tatu ni kusimamia ulinzi na usalama kwa kuweka mikakati ya kudhibiti uhalifu,kipaumbele cha nne ni kusimamia usafi wa mazingira ili kuweka Mkoa katika hali ya usafi pamoja na usimamizi, ufuatiliaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Pia amewataka Wakuu wa Wilaya kutimiza wajibu wao na kutekeleza matarajio chanya ya Rais Samia Suluhu Hassan, kwani amewaamini na ndio maana amewapa nafasi hizo.”Hivyo ukiaminiwa, nawe unatakiwa ujiaminishe ili kuweza kutimiza adhima hii kikamilifu,”amesema Sendiga.
Akizungumza mara baada ya kuapishwa Mkuu wa Wilaya ya Mbulu,Michael Semindu,ameahidi kufanya kazi kwa ushirikiano na watendaji wenzake pamoja na kuyapokea maagizo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa na kuyatekeleza majukumu kwa weledi.
“Si kwamba mimi ni bora kuliko wengine lah hasha, isipokua ni wakati wa Mungu umenifaa mimi kuonekana katika nafasi hii, hivyo nitatekeleza yote aliyoniagiza Mkuu wangu wa Mkoa,” amesema Semindu.
Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Semindu kabla ya kuteuliwa na Rais Dkt. Samia kuwa Mkuu wa Wilaya hiyo, alikua ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Iringa.
More Stories
Premium Active Tanzania yapunguza uhaba wa madawati Mlele
TARURA Kilindi kutumia bil.5.2 bajeti 2025/26
Madiwani Kilindi wapitisha bil.36.8 bajeti 2025/26