Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Wizara ya Maliasili na Utalii imeeleza kuwa inathamini afya ya mama na mtoto kupitia mapato ya utalii yanayotokana na maeneo yaliyohifadhiwa ambapo kwa sasa inachangia asilimia 17 ya Pato la Taifa.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mtoto Njiti Duniani yaliyofanyika katika kijiji cha Robanda Wilaya ya Serengeti mkoani Mara.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo yaliyoambatana na matukio mbalimbali ya wadau kuchangia fedha na vifaa kwa ajili ya kuhudumia watoto njiti yakiongozwa na Taasisi ya Doris Mollel Foundation (DMF), Naibu Waziri Mhe. Mary Masanja ameeleza kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii imekua ikishiriki moja kwa moja katika kuchangia maendeleo katika maeneo mbalimbali likiwemo eneo la afya ya mtoto.
Ameipongeza Taasisi ya Doris Mollel Foundation (DMF) kwa kuweza kuandaa matukio mbalimbali likiwemo la kurusha balloon katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa lengo la kuitangazia dunia kuwa inamtambua na kumthamini mtoto njiti na kuonesha kwamba thamani hiyo inaweza kuonekana kupitia mchango mkubwa wa Sekta ya Utalii hapa nchini.
Sambamba na hilo, ameishukuru taasisi hiyo kwa kutoa vifaa vya kuhudumia watoto njiti vitakavyogawiwa katika Wilaya ya Kwimba na Magu Mkoani Mwanza.
“Nikiwa kama Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mwanza, naishukuru taasisi ya Doris Mollel Foundation kwa kutoa vifaa vitakavyoenda kuokoa maisha ya watoto njiti Kanda ya ziwa” Mhe. Masanja amesisitiza.
Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa mchango wa fedha taslimu kutoka kwenye mshahara wake kiasi cha shilingi milioni 20 itakayotumika kujenga chumba maalum cha kumhudumia mtoto njiti, na pia kwa kutoa vifaa vya kuhudumia watoto njiti vyenye thamani ya shilingi milioni 50.
More Stories
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato
Wambura asikitishwa na makundi CCM Nyakato