January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sekta ya misitu na nyuki kuendelea kuchangia pato la Taifa

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imepanga kuibua mbinu mpya zitakazoiwezesha Sekta ya Misitu na Nyuki kuongeza mapato katika pato la Taifa.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro alipofanya kikao na menejimenti ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwenye ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Utalii jijini Dar es Salaam.

“Tunategemea tuje na mbinu zote za kuongeza mchango wa Sekta ya Misitu na Nyuki kwenye uchumi wa nchi na mojawapo ya mchango huo ni biashara ya hewa ya ukaa (Forest Carbone Trade)”

Amesema Wizara ya Maliasili na Utalii ina mamlaka kamili kwenye kusimamia biashara ya hewa ya ukaa kwa sababu sheria na sera ya misitu iko chini ya Wizara hiyo.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja ameishauri menejimenti ya TFS kuhakikisha inatekeleza mpango wa biashara ya hewa ya ukaa kwa wakati kwa sababu kwa kufanya hivyo itasaidia kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya maliasili na utalii.

Pia, amewataka watendaji hao kufanya kazi kwa kasi ili kuleta matokeo chanya.

“Tuendane na kasi ya utekelezaji wa mpango huu kwa sababu sisi tunapimwa pale tunapoonyesha matokeo chanya kama alivyosema Mhe. Waziri tunaangaliwa tumeingiza fedha kiasi gani na watalii kiasi gani” Mhe. Masanja amesisitiza.

Naye, Mtendaji Mkuu, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo amewapongeza kwa kuteuliwa kwa mara nyingine kuiongoza Wizara na kuahidi kutoa ushirikiano na kuhakikisha anasimamia utekelezaji wa maagizo yote yaliyotolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) (katikati) akizungumza na menejimenti ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Utalii jijini Dar es Salaam leo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) (katikati) akizungumza na menejimenti ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Utalii jijini Dar es Salaam leo. Kulia ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja (Mb) na kushoto ni Mtendaji Mkuu, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ,Prof. Dos Santos Silayo .
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja (Mb) akizungumza na menejimenti ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Utalii jijini Dar es Salaam leo. Kushoto ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akifuatilia.
Mtendaji Mkuu, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo akitoa ufafanuzi wa namna biashara ya ukaa inavyoweza kufanyika katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Utalii jijini Dar es Salaam leo.