March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sekta ya mbolea yaanza kung’aa,Serikali yafungua milango fursa mpya kwa wawekezaji

Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online

MKURUGENZI Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Joel Lawrent, amesema Serikali inaendelea kuwekeza kikamilifu katika kukuza tasnia ya mbolea nchini huku ikiibua fursa lukuki kwa Watanzania na wawekezaji kuwekeza katika kila hatua ya mnyororo wa thamani wa pembejeo hiyo muhimu.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Maonyesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Lawrent alieleza kuwa tayari hatua kubwa zimepigwa katika kuimarisha uzalishaji wa mbolea, hususan baada ya uzinduzi wa kiwanda kikubwa kilichopo eneo la Nala, mkoani Dodoma.

“Tarehe 28 Juni mwaka huu, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alizindua rasmi kiwanda hicho ambacho kina uwezo wa kuzalisha takribani tani milioni moja za mbolea kwa mwaka,hii ni hatua kubwa katika safari ya kujitosheleza kwa uzalishaji wa mbolea nchini,” alisema.

Mbali na kiwanda cha Nala, TFRA imebainisha uwepo wa viwanda vingine kama kile cha Minjingu, ambacho huzalisha takriban tani 250,000 kwa mwaka, na hivyo kuashiria ongezeko la uwezo wa ndani wa kuzalisha mbolea huku akisema hata hivyo, bado kuna fursa kubwa kwa wawekezaji wapya kuwekeza katika uzalishaji, uagizaji, na usambazaji wa mbolea.

Mkurugenzi huyo amesisitiza kuwa mahitaji ya mbolea nchini yanatarajiwa kuongezeka maradufu kufikia mwaka 2030, na kwa sasa matumizi yameongezeka kutoka tani 360,000 mwaka 2023 hadi kufikia takribani tani milioni moja mwaka huu.

“Hili ni ongezeko kubwa na linadhihirisha mwamko wa wakulima katika kutumia mbolea kwa tija. Hivyo tunatoa wito kwa wafanyabiashara na wawekezaji kujiandaa kushiriki kikamilifu katika sekta hii,” ameongeza.

Aidha amesema , TFRA imeanzisha mfumo wa kielektroniki wa usambazaji na uuzaji wa mbolea za ruzuku, unaolenga kuhakikisha mbolea sahihi inawafikia wakulima waliokusudiwa kwa bei nafuu na kwa wakati.

Ametumia nafasi hiyo kuwaasa wakulima wote nchini wajisajili ili waweze kupata na kutumia fursa ya mbolea ya ruzuku iliyotolewa na serikali ili waweze kuzalisha kwa tija mashambani.

Amesema Kupitia mfumo huo, pembejeo kama mbegu na mbolea sasa zinapatikana kwa usimamizi wa karibu zaidi, hatua inayoongeza uwazi na ufanisi.

Serikali pia imeanza kampeni ya kupima afya ya udongo nchi nzima ili kuhakikisha mbolea inayotumika inalingana na mahitaji halisi ya udongo huku akisema hiyo ni fursa nyingine kwa wazalishaji na waagizaji wa mbolea kuzingatia utafiti huo ili kuongeza tija ya kilimo.

Mbali na uzalishaji na usambazaji, fursa nyingine zilizobainishwa ni pamoja na ujenzi wa maghala ya kuhifadhi mbolea, hasa katika maeneo ya vijijini,ufungashaji wa mbolea katika vifungashio vinavyokubalika sokoni (kilo 50, 25, hadi kilo 5 au 10),Teknolojia za ufuatiliaji na usambazaji, kupitia mifumo ya kidigitali

“Tuna viwanda vichache vya kufungasha kwa sasa, lakini tunatarajia biashara ya ufungashaji kuwa kubwa zaidi,hili ni eneo lingine ambalo Watanzania wanapaswa kulitazama kwa makini,” alisema Bw. Lawrent.

Aidha amesema,kupitia banda la TFRA katika maonyesho ya Sabasaba, wawekezaji na wananchi wanapewa elimu kuhusu fursa hizi na namna ya kushiriki katika kuinua sekta ya mbolea ambayo ni uti wa mgongo wa kilimo cha kisasa huku akiwaasa wadau wa kilimo na wananchi kwa ujumla kufika kwenye banda hilo kujionea na kuchukua fursa hizo kwa ajili ya maendeleo yao ya kiuchumi.