Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
NAIBU Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia ,Wanawake na Makundi Maalum Mwanaidi Alli Khamis amezitaka Sekretarieti za Mikoa hapa nchini kwenda kusimamia vyema na kusambaza elimu ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (MMMAM) ili kuhakikisha utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ya miaka mitano (PJT-MMMAM 2021/22-2025/26) unatekelezeka hadi katika ngazi ya Jamii.
Akifungua mafunzo ya Kitaifa ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (MMMAM) yanayoendelea jijini Dodoma yanayolenga katika kuwekeza kwa watoto wenye umri wa miaka sifuri hadi minane,Naibu Waziri huyo amesema sekretarieti za mikoa ndiyo waratibu na wasimamizi wa utekelezaji wa PJT-MMMAM hivyo wanapaswa kwenda kufanya kazi hyo kwa weledi na kuyafikia makundi yote katika kusambaza elimu hiyo ambao inapaswa ifike hadi vijijini ambako kuna changamoto nyingi za malezi.
“Mafunzo haya ni muhimu sana katika malezi na makuzi ya watoto wetu ,elimu hii sasa ikasambae hadi kwa wananchi hadi wale wanaoishi katika maeneo ya vijijini .”amesema Mwahamisi
Amesema,kwa kuwa baada ya mafunzo hayo mikoa yote 26 ya Tanzania Bara itakuwa imeshafikiwa,hivyo matarajio ya Serikali ni ni kuona watoto wanapata malezi ya awali ambayo yatamsaidia mtoto kuimarika ,kujielewa na kuhakikisha anakua vyema na hivyo kuleta tija kwa Taifa hapo baadaye.
“Baada ya mafunzo haya natarajia kuwepo na wengi zaidi katika ngazi mbalimbali na hivyo kuwa na uhakika wa Programu hii kwamba inaratibiwa na kusimamiwa na watu sahihi wenye weledi kuhusu malezi na makuzi na maendeleo ya awali ya watoto.”amesisitiza
Kwa upande wake Naibu katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia ,Wanawake na Mkundi Maalum Wakili Amon Mpanju amesema utekelezaji wa Programu hiyo unahitaji umakini katika usimamizi na uratibu kwa vitendo.
“Kupata mafunzo peke yake haitooshi,nendeni mkasimamie utekel;ezaji wake na kuhakikisha maeneo muhimu katika suala l;a malezi ,makuzi na maendeleo ya awali ya Mtoto yanazingatiwa ambayo ni Afya bora,lishe ya kutosha,malezi yenye mwitikio,ulinzi na usalama wa mtoto pampja na ujifunzaji wa awali.”amesema Mpanju
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mtoto Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Sebastian Kitiku, amesema Wizara itaendelea kushirikiana kwa karibu na wadau wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Mtoto ili kuhakikisha kuna mazingira salama ya ustawi na Maendeleo ya Watoto Nchini.
“Kuwekeza kwa mtoto ni jambo muhimu maana kitaalam,katika umri wa sifuri hadi miaka minane ndilo eneo ambalo ubongo wa mtoto hukua asilimia 80-90,kwa hiyo huu ndiyo umri sahihi wa kuhakikisha mtoto anapata malezi stahiki.”amesema Kitiku
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Shirika linaloangazia masuala ya watoto la Children in Crossfire Frank Samson amesema, Shirika hilo linashirikiana na serikali na Umoja wa Klabu za waandishi wa Habari nchini (UTPC) katika kutekeleza mradi wa Mtoto Kwanza ambao unapelekea utekelezaji wa PJT-MMMAM .
Aidha amesema,takwimu zinaonyesha karibu asilimia 66 ya watoto kusini mwa jangwa la Sahara wapo katika hatari ya kukua bila kufikia utimilifu wao na asilimia 43 yake ipo katika nchi nyingine na Tanzania ikiwemo huku akisema takwimu hioz zinaonyesha bado inahitajika jitihada kubwa kuwekeza kwa watoto wenye umri wa sifuri hadi miaka minane.
Akizunguimza kwa niaba ya Chuo Kikuu cha Aghakan cha Nchini Kenya Profesa Amina Abubakari amesema matarajio yake mafunzo hayo yatakuwa na manufaa makubwa kwa watoto kwa miaka ijayo.
Akitoa neno la shukrani mshiriki wa mafunzo hayo Tedson Ngwale ambaye ni Afisa Maendeleo kutoka mkoani Shinyanga ameishukuru Serikali kwa jitihada hizo za kuhakikisha inaanda mazingira salama kwa watoto kwa kutoa mafunzo hayo.
Washiriki wa mafunzo hayo ni Maafisa Maendeleo na maafisa Ustawi wa Jamii wa mikoa ,Maafisa kutoka Wizara za kisekta pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali kutoka mikoa 16 ya Tanzania.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakani
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best