November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma yatoa elimu maonyesho Nane Nane

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

OFISI ya Sekretarieti ya Ajira na Utumishi wa Umma imeyatumia maonyesho ya wakulima Nane Nane kutoa elimu kwa wananchi ya namna ya kutumia mfumo wa Ajira Portal katika kuomba ajira.

Akizungumza na waandishi wa habari katika banda la ofisi hiyo kwenye maonyesho ya wakulima yaliyofanyika  jijini Mbey,katika Viwanja vya John Mwakangale,Geofrey Kikosa kutoka Ofisi ya Sekretarieti ya Ajira na Utumishi wa Umma amesema,wameweza kukutana na wateja/wadau ambao wamefika kwenye banda lao na kuwaelimisha kufanya mchakato huo.

“Katika maonyesho ya haya Nane Nane tumekutana na wadau kusikiliza changamoto wanazokabiliana hasa wakati wa uombaji wa ajira hadi wakati wa usaili,na baada ya kuwasikiliza pia tumewasaidia kutafuta suluhu ya changamoto zao pamoja na kupata maoni ya wadau kuhusu  mchakato wa ajira unavyoendeshwa.”amesema Kikosa na kuongeza kuwa

“Wadau wengi waliojitokeza kwenye banda letu  wameonyesha kuhitaji msaada katika eneo la usajili na sisi  tumewaelekeza ukubwa wa picha unaotakiwa uwekwe na kuwaelekeza namna ya kufanya usajili vizuri katika akaunti zao ikiwemo kuhakiki vyeti vyao kwa mawakili au wanasheria.”

Vile vile amesema wamepata maoni katika eneo la kushindwa kuomba nafasi mbalimbali zinazotangazwa katika taasisi mbalimbali ambapo wameitumia changamoto hiyo kama fursa ya kutoa elimu zaidi katika eneo hilo.

“Wadau wengi wamekuwa na sifa za juu na tumekuwa tukiwaelekeza waombe nafasi kwa mujibu wa kiwango cha elimu ya nafasi inayotangazwa,pia tumepata changamoto ya wadau kusahau neno la siri na tumewaelekeza namna  ku-‘reset’ hilo  neno siri ili kupata neno siri jipya.”amesisitiza

Amewaasa wadau na waombaji ajira katika utumishi wa umma kufika katika ofisi zao au kutembelea tovuti yao ili kuona maelekezo ikiwemo kupata  namba za simu kwa ajili ya kupiga na kupata huduma wanazozihitaji.

“Baadhi ya waombaji wamekuwa wakiomba kwa kutumia elimu ya juu kuliko inayotangazwa ,lakini katika maonyesho ya Nane Nane kuwaeleza kuwa maombi yanapaswa kuombwa kwa ngazi ya elimu inayotangazwa kwa sababu mchakato huu hufanywa kwa kuzingatia kiwango cha elimu kinachotakiwa ili tuwapime wahusika wenye kiwango kimoja cha elimu na bila upendeleo.”alisema Kikosa

Akizungumzia kuhusu mchakato wa ajira unavyoendeshwa  alisema mchakato huo unaendeshwa na kuchagua waombaji kwa kuzingatia maadili weledi pamoja na sifa na vigezo vya waombaji wa nafasi husika.

Aidha alisema,katika kuendesha mchakato huo ofisi yao hushirikiana na waajiri na wataalam mbalimbali kwa lengo la kuufa nya mchakato kufanyika kwa uwazi na kuzingatia vigezo vinavyohitajika.