April 19, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sekondari mpya nne kufunguliwa Aprili,2025 Musoma Vijijini

 

Fresha Kinasa,TimesMajiraOnline,Mara.

JUMLA ya Sekondari mpya nne zinatarajiwa kufunguliwa ndani ya mwezi huu wa  Aprili,2025 katika Jimbo  la Musoma Vijijini ambazo zitasaidia kuondoa changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kwenda masomoni na  kuleta ufanisi katika masomo yao kwa kusoma karibu na nyumbani.

Kuzinduliwa kwa shule hizo, ni neema na jambo la furaha kwa Wananchi wengi jimboni humo wakiona mafanikio yao kutokana na kujitolea kwao michango na nguvu kazi zao. Wakiongozwa na Mbunge wao Prof. Sospter Muhongo ambaye amekuwa bingwa katika kuleta mageuzi ya maendeleo ya nyanja mbalimbali jimboni humo. 

Hayo yameelezwa Aprili 18, 2025 kupitia Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya  Mbunge waJimbo la Musoma Vijijini ambapo imesema kuwa, “Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof Sospeter Muhongo, anawakaribisha wanafunzi, wazazi na wanavijiji kwenye sherehe za kufungua sekondari mpya nne za Jimboni mwetu.” imeeleza sehemu ya Taarifa hiyo na kusema.

“Ratiba ya Ufunguzi wa sherehe,Mgeni Rasmi ni Mkuu wa Wilaya ya Musoma. Ambapo Butata Sekondari, Kijijini Butata, Kata ya Bukima Alhamisi ya tarehe 24.4.2025, Saa 6:30 mchana.  Sekondari ya Kumbukumbu ya David Massamba, Kijijini Kurwaki, Kata ya Mugango Ijumaa,Aprili 25,2025, Saa 6:30 mchana. Na  Muhoji Sekondari, Kijijini Muhoji, Kata ya Bugwema Jumatatu, ya Aprili 29,2025
Saa 6:30 mchana.”imeeleza taarifa hiyo.


Pia, Nyamrandirira Sekondari ya Amali Kijijini Kasoma, Kata ya Nyamrandirira ni jumanne ya tarehe 29. 4. 2025 saa 6:30 mchana,  na mgeni rasmi atakuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi.

Pia Taarifa hiyo imefafanua kuwa, ujenzi wa Sekondari nyingine Mpya unaendelea kwenye Vijijini vya Nyasaungu, Kata ya Ifulifu,  Kisiwani Rukuba, Kata ya Etaro Kijijini Mmahare, Kata ya Etaro,  Kiriba, Kata ya Kiriba,Kataryo, Kata ya Tegeruka,  Nyambono, Kata ya Nyambono, Musanja, Kata ya Musanja na  Chitare, Kata ya Makojo.

Amewataka Wananchi jimboni humo na wadau mbalimbali wa maendeleo kujitokeza kuchangia ujenzi wa shule za awali (shikizi) Msingi na Sekondari Jimboni humo.

Kwa upande wao Wananchi ndani ya Jimbo hilo, wamesema juhudi za pamoja  na Mbunge wao zimeendelea kuzaa matunda na kuleta mafanikio hasa katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya elimu ambayo imekuwa na tija kubwa ikiwemo ya  ujenzi wa maabara, madarasa  na shule. 

“Namshukuru Mbunge wetu kwa juhudi kubwa za utoaji wa  michango yake kupitia harambee ambazo amekuwa akiziendesha jimboni, bidii ya ufuatiliaji, na usimamizi madhubuti umeleta matokeo chanya na tunafurahi tunazindua shule Mpya nne ambazo ni chachu ya ufaulu wa Watoto wetu.”amesema Juma Masige.

Sekondari za kata/serikali katika Jimbo la Musoma Vijijini ni 26, na Sekondari za madhehebu ya Dini 2, na Sekondari mpya nne zinazinduliwa ndani ya  mwezi huu katika Jimbo hilo lenye kata 21 zenye Vijiji 68.