Na Mwandishi Wetu
Baraza la Ushindani (FCT) la Tanzania limefutilia mbali uamuzi wa Tume ya Ushindani (FCC) uliotolewa Februari 28 mwaka huu wa kuiruhusu Scancem International Da kutwaa asilimia 68.33 ya hisa za Tanga Cement PLC bila masharti yoyote.
Katika uamuzi wake wa Oktoba 16, 2023, FCT chini ya uenyekiti wa Jaji Fatma Maghimbi, iliamua kwamba madhali FCT ipo kwa ajili ya kusimamia na kurekebisha mwenendo na uamuzi wa FCC, haikuwa sahihi kuwapo maamuzi mawili yanayopingana kutoka kwenye vyombo hivyo katika suala moja, ikizingatiwa FCT ilipata awali kuzuia muungano wa kampuni hizo.
Jaji Maghimbi aliyeshirikiana na wajumbe Dr Onesmo M. Kyauke na Dk. Godwill G. Wanga walisema haiwezekani chombo kilicho kikubwa zaidi (FCT uamuzi wa Aprili 6, 2022) kwenye suala hilo hilo upingwe na chombo kilicho kidogo zaidi (FCC).
Walikuwa wanatoa uamuzi kwenye shauri lililofunguliwa na Peter Hellar dhidi ya FCC, Scancem International DA, Fayaz Bihojani, Wiilliam Erion a Hakan Gurdan, kutaka wajibu maombi wajieleze mbele ya baraza hilo, kwa nini wasichukuliwe hatua kwa kulidharau baraza katika maamuzi yake.
Hata hivyo, Jaji Maghimbi na wajumbe wa FCT walisema wajibu maombi si wa kulaumiwa kwa kilichotokea, japokuwa ni kweli kwamba maamuzi mawili tofauti hayawezi kusimama kwenye soko moja.
“Swali linabaki, kipi kifanyike? Bw Deodatus Nyoni, Wakili Mwandamizi wa Serikali akiiwakilisha FCC alipendekeza kwamba ili kupata suluhu ya hali husika, Baraza lifute uamuzi wa FCC wa Februari 28, 2023 na kutoa ruhusa kwa wajibu maombi kuwasilisha upya ombi la Baraza kupitia upya uamuzi wa Baraza hili wa Septemba 23,2022,” wakasema kwenye uamuzi uliosomwa na Jaji Maghimbi.
Wakihitimisha, walikubaliana na wakili huyo, wakisema kwamba baraza hilo halipo kwa nia ya kuvuruga FCC wala kuchelewesha wawekezaji tarajiwa, bali kulinda na kukuza ushindani kwenye biashara na kulinda walaji, walisema muda uliotumiwa kuwasilishwa kwa ombi jipya la utwaaji hisa ulikuwa mfupi mno, hivyo kwamba hawadhani mazingira ya uchumi, biashara yalikuwa yamebadilika, wakaongeza kwamba angalau kiwe kipindi cha mwaka mmoja.
Kwa msingi huo, FCT ilibatilisha ombi la kuungana kampuni husika namba CBC. 127/359/144.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja