September 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

SBAN, RVO na Ubalozi wa Uholanzi wazindua programu ya kuwafundisha wawekezaji wadogo

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

MTANDAO wa wawekezaji kwenye kampuni changa (SBAN) kwa kushirikiana na Ubalozi wa Uholanzi na Wakala wa Biashara wa Uholanzi (RVO) wamezindua rasmi kundi la pili la programu ya kuwafundisha wawekezaji wadogowadogo jinsi ya kuwekeza kwenye kampuni changa ( Tanzania Angel Investors Accelerator) lengo ni kuongeza idadi ya wawekezaji wa ndani na kuvutia mitaji ya kigeni kwenye mfumo wa ikolojia wa kuanzia Tanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari , Mwanzilishi na Meneja wa mtandao kutoka mtandao huo wa SBN , Rodrique Msechu alisema Baada ya awamu ya kwanza ambayo ilifanyika mwezi Novemba 2023 walifanikiwa kupata dola 30,000 kutoka kwa wawekezaji na kupelekea kuwekeza kwenye kampuni changa 3.

Alisema katika uwekezaji wa mwaka 2027, wanatarajia kuwafikia watu 25 na kuwekeza zaidi ya dola milioni 1 kutoka nchini Tanzania.

“Leo hii tunafurahi kwamba ubalozi wa uholanzi wametupa msaada wa kuweza kufanya progrmu hii tena lengo ni kuwa na wawekezaji wadogowadogo kwenye kampuni changa ambao wanaweza pale ikifika 2027 kuwekeza zaidi ya dola milioni 1 kutoka hapa Tanzania”

Aidha Msechu alisema ili mtu ashiriki
Katika programu hiyo, atahitajika awe mtu ambaye unafanya kazi kwenye taasisi na unauwezo wa kuwekeza kima cha chini Dola 1000 na kutoa kiingilio cha Dola 200

“Programu hii ili kushiriki unahitaji uwe mtu ambaye unafanya kazi kwenye taasisi na unauwezo wa kuwekeza kima cha chini Dola 1000

Hivyo ili uweze kuingia kwenye programu tutahitaji uweze kuahidi kwamba utawekeza dola 1000 na kiingilio utalipa Dola 200” Alisema

Bw. Francis Omorojie, mwanzilishi mwenza wa mtandao huo wa SBAN and Ennovate Ventures, alionyesha kufurahishwa na uzinduzi huo, akisema, “Hii ni hatua nyingine ya kujivunia ya SBAN katika kuongeza kasi ya uhamasishaji wa mitaji ya ndani kwa ajili ya kuanza kwa Tanzania. Tumejitolea kuongeza idadi ya wawekezaji wa ndani wa malaika na kuwapa ujasiri na rasilimali kufanya uwekezaji wenye matokeo.”

Profesa Faustin Kamuzora, mshiriki wa kundi la kwanza la programu ya Tanzania Angel Investors Accelerator (TAA ), alisisitiza umuhimu wa uwekezaji huo ili kutengeneza utajiri wa muda mrefu.

“Ingawa nina uzoefu katika nafasi ya uwekezaji, programu ya TAA ilinipa zana muhimu na kuniunganisha na jumuiya ya wawekezaji. Mtandao huu unawawezesha washiriki kuondoa hatari ya uwekezaji kwa kuwekeza kiasi kidogo na kubadilisha fedha zao.”

“Nilibahatika kushiriki kwenye mafunzo ya kwanza ya kuwafundisha uwekezaji katika makampuni madogomadogo ambayo yanakuwa na mawazo makubwa lakini wakati mwingine wanakuwa na changamoto ya mitani, mimi nimeingia kwasababu pamoja na uzoefu wangu wa kuwekeza katika sekta mbalimbali,”

Aidha alizitaja faida za programu hiyo huku akibainisba mchakato wa kupatikana kwa mawazo yaliyo bora zaidi ambayo yataleta manufaa pale mwekezaji anapotaka kuwekeza katika wazo hilo.

“Faida ya programu hii ni kwamba kama hilo wazolinahitaji milioni 10, kwa kuunganika pamoja inakuwa wawekezaji mnachangia kwasababu haya makampuni madogomadogo hayo mawazo mara nyingi yana vihatarishi vikubwa kwamba si lazima ukiwekeza upate faida sasa unapunguza ile kihatarishi au riski unapochangia na wenzako”

Alisema “Kuna mchakato wa kuona kama hili wazo ni zuri pamoja na kwamba hilo wazo linakua limechakatwa lakini kwakuwa bado linakuwa halijaingia sokoni, uwezekano wa kupoteza pesa ni mkubwa”

Kamuzora aliendelea kusisitiza wawekezaji wengine kuendelea kushirikiana kwa pamoja kwani yapo mawazo ambayo hapo baadaye yanakuja kufikia malengo .

“Kwa hiyo na sisi Tanzania tukiwa na uwezo wa kuweka pamoja wawekezaji, na mitaji kuna mawazo mengine yatakuja kutoka kwahiyo cha kusaidia ni kwamba sera yetu ya uwekezaji itahitaji angalau itambue sana jukumu la uwekezaji katika biashara zinazoanza”

John Mike Jager, Mkuu wa Idara ya Uchumi katika Ubalozi wa Uholanzi nchini Tanzania, alisema kwamba ubalozi wa Uholanzi umekuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono mfumo ikolojia wa Startup na anafurahi kwamba Kundi la 2 la TAA litaangazia uwezo ambao haujatumiwa katika uwekezaji wa malaika nchini Tanzania.