January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

SAUT na Regional Aviation & Business College,wasaini makubaliano kutoa mafunzo kwa vitendo sekta ya usafiri wa anga wa kiraia

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

Katika kuhakikisha sekta ya anga ya kiraia nchini inakua na kuacha kutegemea wataalamu kutoka nje,vijana nchini wanapaswa kusomeshwa ili waweze kuona fursa za kuingia na kuwekeza katika sekta hiyo.

Hivyo ili kufikia malengo hayo Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (Saut) jijini Mwanza na Regional Aviation & Business College wamesaini makubaliano ya kuwafundisha kwa vitendo wanafunzi wa chuo kuhusiana na usafiri wa anga wa kiraia.

Akizungumza mara baada ya kusaini makubaliano hayo baina ya pande hizo mbili Makamu Mkuu wa SAUT Profesa Costa Mahalu ameeleza kuwa makubaliano hayo ni ya miaka mitano ambayo yanaaza kuanzia Leo Julai 29,2022 lengo ikiwa ni kuwawezesha wanafunzi kupata ujuzi kwa vitendo .

Prof.Mahalu ameeleza kuwa wameona wapige hatua kwa kushirikiana na wenzao hasa kwenye masuala ya usafiri wa anga wa kiraia ili wanachuo wajifunze kabla hawajaingi kwenye ajira.

Ameeleza kuwa pia wanafunzi wanaomaliza degree zao katika fani ya uhandisi au fani mbalimbali katika ushirikiano wao wanaweza kwenda kusomea kwa vitendo fani mbalimbali katika masuala ya anga kwa kukishirikiana na wenzao ambao wameingia nao makubaliano.

“Tukishirikiana kuna nyanja mbalimbali zitafunguka,wanachuo watajifunza hasa kivitendo na wakihitimu watakuwa wametanua wigo wa ajira ndani na nje ya nchi,wanafunzi wa fani mbalimbali nao watapata fursa ya kusoma kozi mbalimbali zilizopo za usafiri wa anga,”ameeleza Profesa Mahalu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chuo cha Regional Aviation & Business Captain Phillemon Kisamo, ameeleza kuwa kozi za usafiri wa anga azifahamiki sana nchini hivyo wameona washirikane na chuo hicho kwa kuwa ushirika wao ni nafasi nzuri ya kutoa fursa kwa vijana waTanzania kujifunza kuhusu sehemu hiyo ambayo ni muhimu ya kukuza uchumi katika ulimwengu.

Capt.Kisamo ameeleza kuwa kuna mambo mengi ya kujifunza na yakawapeleka kwenye ulimwenguni kufanya kazi ,wanahitaji kuwafundisha vijana wa Tanzania ili wawe na ujuzi wa kujiajiri na kuajiriwa pamoja na kukuza sekta ya usafiri wa anga,kupata ajira nje ya nchi mara baada ya kuhitimu na kupata vyeti kwa nasomo watakayoyafanya.

“Uchumi wa Tanzania unakuwa kwa kasi na sekta ya anga nayo inakuwa na ukanda wa Afrika Mashariki kuna fursa nyingi za kupata ajira na kuanzisha shughuli ni nafasi nzuri ya sisi kuwa na mahusiano na chuo cha Saut ili kuweza kuwezesha vijana wetu wa Tanzania waweze kuwa na nafasi nzuri ya kufanikiwa katika uchumi hasa tukiangazia sekta ya usafiri wa anga,”ameeleza Capt.Kisamo.

Pia ameeleza kuwa kuna watu wachache sana ambao wanaweza kuendesha shughuli za anga nchini,ambapo katika uendeshaji wa ndege kwa maana ya marubani na mafundi wengi wametoka nje ya nchi,hivyo hawawezi kukuza sekta ya usafiri wa anga wa kiraia kwa kutegemea watu kutoka nje tu.

“Hatuwezi kukua kama vijana hawajasomeshwa katika sekta hiyo na kuona fursa ya kuingia ili wawekeze mawazo yao na mbinu zao ili na wao waanzishe vitu ambavyo vinaweza kuleta matokeo makubwa katika sekta ya anga,tunaona hii ni fursa nzuri ya kuwa pamoja ya kuwawezesha vijana wetu katika usafiri wa anga,” ameeleza.

Kwa upande wake Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma- Saut Prof.Hossea Rwegoshora anaeleza kuwa hiyo ni fursa kwao kwa sababu uchumi unakua na usafiri wa anga ni kiwanda kinachokuwa kwa kasi nchini.

“Kwa bahati mbaya sana vyuo vikuu vilikuwa vikiambiwa kwamba vinatoa ujuzi elimu kwa wahitimu wetu lakini watu hawaajiriki hivyo sasa tunatafuta muunganiko kati ya vyuo vikuu na viwanda ili wanachokisoma hapa shuleni waweze kuyafanyia mazoezi kwa vitendo katika maeneo hayo na baadaye waweze kufanya kazi katika maeneo yaleyale .” anaeleza Rwegoshora

Ameongeza kuwa lengo likiwa elimu wanayoitoa iweze kuwasaidia wahitimu wao kuweza kuajirika na kuleta faida kwa watanzania walio wengi.

Makamu Mkuu wa SAUT Profesa Costa Mahali,akisaini makubaliano ya kuwafundisha kwa vitendo wanafunzi wa chuo kuhusiana na usafiri wa anga wa kiraia baina ya chuo hicho na chuo cha Regional Aviation & Business,hafla iliofanyika chuoni SAUT jijini Mwanza.(Picha na Judith Ferdinand)
Mkurugenzi Mtendaji wa chuo cha Regional Aviation & Business Captain Philemon Kisamo akisaini makubaliano ya kuwafundisha kwa vitendo wanafunzi wa chuo kuhusiana na usafiri wa anga wa kiraia baina ya chuo cha SAUT na chuo cha Regional Aviation & Business,hafla iliofanyika chuoni SAUT jijini Mwanza.(Picha na Judith Ferdinand)
Makamu Mkuu wa SAUT Profesa Costa Mahali(kulia) akishikana mikono na Mkurugenzi Mtendaji wa Chuo cha Regional Aviation & Business, Capt.Philemon Kisamo mara baada ya kusaini makubaliano ya kuwafundisha kwa vitendo wanafunzi wa chuo kuhusiana na usafiri wa anga wa kiraia baina ya chuo hicho na chuo cha Regional Aviation & Business,hafla iliofanyika chuoni SAUT jijini Mwanza.(Picha na Judith Ferdinand)
Makamu Mkuu wa SAUT Profesa Costa Mahali,akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani kabla ya kusaini makubaliano ya kuwafundisha kwa vitendo wanafunzi wa chuo kuhusiana na usafiri wa anga wa kiraia baina ya chuo hicho na chuo cha Regional Aviation & Business,hafla iliofanyika chuoni SAUT jijini Mwanza.(Picha na Judith Ferdinand)