March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

SAU kuimarisha sekta ya kilimo, teknolojia na viwanda

“Kuweka mfumo madhubuti kutambua vipaji vya vijana

*Kuwezesha Watanzania kumiliki asilimia 30 ya hisa kwenye miradi mikubwa ya maendeleo

*SAU yazindua kampeni jijini Dar-es-Salaam

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Dar

MGOMBEA wa kiti cha Urais kupitia chama cha Sauti ya Umma (SAU), Majalio Kyara, amesema kuwa endapo atapewa ridhaa ya kuongoza taifa katika uchaguzi , atahakikisha anaimarisha sekta ya teknolojia, kilimo na viwanda sambamba na kuweka mfumo madhubuti wa kutambua, kulea na kukuza vipaji vya vijana kwa ajili ya maendeleo ya taifa.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kampeni za chama hicho uliofanyika Ukonga Mombasa, Kyara amesema kuwa Tanzania ina vijana wengi wenye vipaji vinavyopotea kwa sababu ya kukosa mfumo rasmi wa kuwaendeleza.

“Mfano mzuri ni kijana aliyemaliza kidato cha sita kutoka Kimara ambaye amejitolea kufundisha kwa moyo. Vijana kama hawa wanapaswa kuungwa mkono, si kupuuzwa,” amesema Kyara.

Akizungumzia sekta ya kilimo, amesema kuwa kilimo hai kimepewa kipaumbele katika ilani ya SAU kwa sababu ni msingi wa afya bora, ajira na ustawi wa jamii.

“Kilimo ni kama damu katika mwili wa binadamu. Tutahamasisha kilimo hai ili Watanzania wale chakula bora na kuimarisha afya ya jamii,” amesisitiza.

Kuhusu uchumi wa nchi, Kyara amesema chama chake kitaweka mazingira yatakayowezesha Watanzania kumiliki asilimia 30 ya hisa kwenye miradi mikubwa ya maendeleo ili kuwapa uwezo wa kushiriki kikamilifu katika uchumi wa taifa.

“Tunahitaji mifumo ya kiuchumi inayompa nafasi mzawa. Uchumi wa Taifa lazima ushikwe na Watanzania,” amesema Kyara.

Aidha, amebainisha kuwa chama hicho kitalenga kuanzisha kongani za viwanda kila mkoa, ikiwa ni mkakati wa kuongeza uzalishaji, ajira na mchango wa nchi katika kulisha Afrika nzima.

Sanjari na hayo,Kyara ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kumpigia kura ya ndiyo, akiahidi kuongoza kwa misingi ya utawala bora, maadili, hofu ya Mungu na kusimamia rasilimali kwa maslahi ya Watanzania wote.