
Na Mwandishi Wetu
Mkurugenzi wa Utawala Hospitali ya Besta, iliyopo Kinondoni Mkoani Dar es Salaam, Dkt. Reuben Mringo amesema kuwa juhudi za kutibu wagonjwa wa saratani hazitumii tiba ya dawa peke yake bali ni pamoja na huduma za ushauri wa kisaikolojia kutoka kwa madaktari, wahudumu wa afya, familia na marafiki.
Akizungumza katika uzinduzi wa siku ya Mashujaa wa Saratani nchini, Jumatano wiki hii, Dkt. Mringo alisema hospitali ya Besta imekuwa ikitumia mtindo huo na umesaidia wagonjwa wengi wa saratani kupona mapema.
“Unajua wagonjwa wengi wa saratani hupata msongo wa maisha kwamba kuugua saratani ni kufa. Tena wengi wakiandikiwa tiba ya mionzi, huamini kuwa anayepatiwatiba hiyo hufa,” alisema Dkt. Mringo akifafanua:
“Nawahakikishia tiba ya mionzi ni salama na husaidia wagonjwa wengi ila kinachochochea wagonjwa wengi wa saratani kuzidiwa na hata kufa ni msongo wa mawazo na hata kukimbia tiba sahihi hospitalini.”
Alisema hospitali ya Besta ina mfumo maalumu wa kuwatibu wagonjwa kisaikolojia kwa kuwaelimisha juu ya ugonjwa walio nao, umuhimu wa tiba wanazozitoa, jinsi ya kuishi kwa amani na matumaini ya maisha baada ya tiba.
Daktari Bingwa wa Saratani Hospitali ya Besta, Dkt. Mpibalema Yemela alisema kuwa tiba za saratani mara nyingi huwa ni za muda mrefu, hadi miaka mitano, inabidi kuwapatia elimu ya saikolojia pamoja na familia na hata marafiki.
Mratibu wa Huduma za saratani Hospitali ya Besta, Dkt. Ismail Dauda, alisema hospiutali hiyo ina vifaa vya kisasa vya uchunguzi pamoja na tiba hivyo kwa sasa hakuna haja ya mgonjwa kupelekwa nje ya nchi kwa hofu ya kutopata uchunguzi na tiba sahihi.
“Kitengo cha tiba ya saratani kimejitosheleza kwa huduma zote na tuna mpangilio mzuri wa kuhakikisha hakuna mgonjwa anakaa kwenye foleni muda mrefu kusubiri huduma.
Akizindua siku hiyo ya mashujaa wa saratani hapa nchini, Mkurugenzi wa Taasisi ya Shujaa Foundation, Gloria Kida alisema wagonjwa wa saratani hupitia changamoto nyingi sana baada ya kugundulika.
“Sisi huwa tunawaeleza wasikate tama kuna maisha baada ya tiba hivyo wasikate tamaa. Huwa tunawaambia wanapaswa kusheherekea maisha kama ilivyo katika jamii huwa wanasheherekea siku ya kuzaliwa.
“Katika maadhimisho ya mwaka huu, kama ilivyokuwa mwaka jana, tunaendelea kuhamasisha washeherekee maisha, wafurahi na wajiamini kuwa ni washindi. Waamini kuugua saratani siyo mwisho wa maisha na wapo wengi ambao wamepona na wameishi zaidi ya miaka 25.”
Alielezea kuwa maadhimisho ya mwaka huu yataadhimishwa jijini Dar es Salaam Jumapili ijayo kwa matembezi ya kilomita tano hadi 15 na baadae kukutana na kubadilishana uzoefu pamoja na nasaha kutoka kwa viongozi wa serikali na wataalamu wa afya.
More Stories
TAKUKURU yanasa watuhumiwa wa wizi wa mali za wakulima
CCM yampongeza Rais Samia kutunukiwa tuzo na Bunge
Mwenge wazindua Miradi saba Temeke