November 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sanai Medical Supply waiomba Serikali iwasaidie kulipwa fedha zao

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

MKURUGENZI wa kampuni ya Sanai Medical Supply, inayojihusisha na usambazaji wa vifaa tiba, Juma Selemani Sanai ameiomba serikali kumsaidia kupata Fedha zake zaidi ya shilingi Milioni 100 kutoka Kampuni ya African Inland Logistics Company.

Akizungumza na waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam jana, Sanai amesema wamekuwa wakifuatilia fedha hizo tokea mwezi wa tano hadi wa 10 mwaka huu, bila mafanikio.

Hata hivyo waliamua kuripoti Polisi kwa RB Namba CDS/RB/4285/2023, CDS/IR/2818/2023 ya kujipatia Mali kwa njia ya Udanganyifu baada ya kugundua kuwa kampuni hiyo inachukuliwa na Mwekezaji mwingine.

Aidha, amesema wamekuwa wakidai fedha hizo lakini uongozi wa kampuni hiyo umekuwa ukiwazungusha ukizingatia na wao wanadaiwa sehemu walikochukulia mizigo.

“Tumepata taarifa kuwa ifikapo Desemba 1, mwaka huu kampuni Mpya itaingia na wao kuondoka hivyo tutakosa wa kumdai jambo ambalo linachangia kutuzungusha.

“Tumekuja kuripoti Polisi Ili serikali itusaidie sisi wazawa ambao tunataka kutapeliwa na Kampuni hiyo ya Wahindi,” amesema Mkurugenzi Sanai.

Ameiomba serikali kuhakikisha wao kama wawekezaji wazawa wanapatiwa haki zao na hatua zichukuliwe Kwa kampuni hiyo kuanzia uhalali wake wa kufanya kazi hapa nchini.

“Sisi tumefanya kazi Kwa muda mrefu na Kampuni hii bila vikwazo ila toka umeingia uongozi Mpya akiwemo mhasibu Dinesh wamekuwa wakitusumbua sana kwenye malipo pindi tunapofika kudai Fedha zetu.

“Mpaka sasa imefikia zaidi ya Milioni 160 kutokana na makubaliano ya mkataba kuwa ucheleweshwaji wa malipo Kwa mwezi mmoja kutaongezeka kima Cha fedha Kwa asilimia 23” ameongeza Sanai.

Kuhusu kuripoti Polisi Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, ACP Gabriel Pupa alikiri kuwa malalamiko hayo yameripotiwa kituoni hapo Novemba 27/2023.

Aidha, amesema walalamikiwa waliitwa Novemba 28/2023 na kuhojiwa na kitengo Cha upelelezi ambapo Novemba 29/2023 mlalamikaji na mlalamikiwa walifika kituoni hapo na kukubaliana kulipa fedha hiyo kabla hawajaondoka nchini.

Gazeti hili lilimtafuta Mhasibu wa Kampuni ya African Inland Logistics, Dineshkumar ambaye ndiye aliyehudhuria Polisi kituo ca Kati jijini Dar es Sakaam, lakini simu yake ilikuwa inaita bila ya majibu.

Kwa upande wake, Terminal Meneja wa Kampuni hiyo, Vivek Makundi alisema yeye sio mmiliki wa Kampuni ya African Inland Logistics, hivyo hawezi kuongelea chochote.